Mgombea
urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema mwaka huu ni
wa mabadiliko ili kuiokoa nchi na madeni mengi ambayo yanasababisha
uchumi kuyumba.
Lowassa
ambaye ameambatana na Waziri Mkuu wa mstaafu wa awamu ya tatu,
Frederick Sumaye, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha,
aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na viongozi
wengine, walianza ziara yao ya kampeni za kuomba kura kwa wananchi
Jumatatu wiki hii.
Ziara
ya mgombea urais huyo zilianzia Mkoa wa Iringa ambako alizungumza na
maelfu ya wananchi kwenye mikutano ya hadhara katika majimbo ya Kilolo,
Mufindi na Iringa mjini na jana (Jumanne) aliwasili katika Mkoa wa
Njombe na kuzungumza na wananchi wa majimbo ya Makambako na Njombe
mjini.
Akizungumzia
deni la taifa, Lowassa alisema atakapoingia madarakani atakuwa na kazi
ya kulipa madeni yaliyolimbikizwa ambayo hata haijulikani yametokana na
nini.
Alisema
Rais Benjamini Mkapa alipoingia madarakani alipunguza deni alilolikuta
likawa chini ya Sh. trilioni 10 lakini leo zimefikia zaidi ya Sh.
trilioni 35.
“Kwa
hiyo anayeingia madarakani itabidi aanze kutumia zile fedha ambazo
zingetumika kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania kulipa madeni. Deni la
taifa ni kubwa na hizo fedha tunazodaiwa tujiulize zimefanya nini na
ziko wapi,” alisema.
Alisema
CCM wameanza kufilisika kutokana na kueneza taarifa zisizokuwa za kweli
kwamba Chadema haina ilani wakati ilani hiyo ilizinduliwa mapema
mwishoni mwa wiki iliyopita.
“CCM
wana macho lakini hawaoni, wana masikio hawasikii, tumetengeneza ilani
kiboko ambayo ndani ya miaka mitano nchi itapaa kimaendeleo,”alisema.
Alisema
wananchi wasitishwe na propaganda kwamba wakichagua upinzani damu
itamwagika na nchi itaingia katika vita kwani hakuna Mtanzania
atakayemwaga damu na kwamba nchi itakuwa tulivu labda wao ndio
waivuruge.
Kuhusu
mgogoro kati ya wafanyabishara na TRA kuhusiana na mashine za EFD,
alisema kama atapewa ridhaa na wananchi na kufanikiwa kuingia Ikulu
atalishughulikia haraka suala hilo.
Kuhusu
michango, michango yote isiyokuwa ya msingi katika shule za sekondari
ataifuta hasa ikizingatia kuwa ilani ya uchaguzi ya Chadema imeeleza
bayana kwamba elimu itakuwa bure kwa sababu fedha zipo.
Alisema atahakikisha analinda maslahi ya wafanyakazi wakiwamo walimu ambao wamekuwa wakidai madeni yao bila mafanikio.
Aliongeza kuwa miaka 50 ya utawala wa CCM imetosha na kuwataka watu wanaoogopa kuondoka CCM waache uoga waondoke.
“Wapo wafanyabiashara wanaogopa kwa sababu wanatishwa, nawaambia msiogope. Neno usiope limeandikwa mara 360 ndani ya Biblia,”alisema.
Kwa
upande wa Sumaye wakati akimnadi Lowassa alisema mawaziri wa serikali
hawawezi kupata ujasiri wa kupambana na rushwa kwa sababu mambo machafu
yote yanayofanywa ndani ya serikali yao wanayafahamu.
Alisema
mawaziri waliopo katika serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
wasiwadanganye Watanzania kwamba wanaweza kupambana na rushwa kwa sababu
hawana dhamira ya kweli kwani mambo mengi machafu yanayofanyika ndani
ya serikali wanayafahamu.
“Leo
Magufuli (mgombea urais CCM) anasimama na kusema akiingia Ikulu
atapambana na rushwa hivi yeye yupo wapi si sehemu ya serikali na
ameshindwa kufanya hivyo, amekuwa waziri kwa miaka mingi hakuweza leo
hii akiingia Ikulu ataweza wapi,”alisema.
Katika
hatua nyingine, umetolewa ufafanuzi kuhusiana na taarifa iliyoeleza
kimakosa kuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa, atafuta Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pindi
akiingia madarakani na kuligeuza kuwa la kutoa mafunzo ya ufundi stadi
na kufundisha uzalendo kwa vijana.
Usahihi
ni kwamba katika mkutano wake wa kampeni mkoani Iringa juzi, Lowassa
aliahidi kuingiza mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wanaojiunga JKT
ambako pia wataendelea kufundishwa uzalendo ili waje kulitumikia vizuri
taifa lao; na siyo kufuta JKT.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni