(PRESS RELEASE).
WIZARA
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kwa
masikitiko makubwa na inataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wazazi
wawili tofauti wanaotuhumiwa kuwaozesha watoto wao wa umri wa miaka 13
na kuwakatisha masomo katika mkoa wa Shinyanga na Dodoma.
Imeelezwa
kuwa, wakati mtoto mmoja mwanafunzi wa shule ya msingi Wishiteleja
wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ameozeshwa kwa nguvu kwa mahari ya
ngombe 13 na kumkatisha masomo yake akiwa darasa la sita, mtoto mwingine
wa mtaa wa Chikole, Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma anasemekana
kuozeshwa kwa mahali ya shilingi 600,000. Kufuatia kuwepo kwa matukio
haya mawili Wizara inataka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Kamati za
Ulinzi wa Mtoto katika mikoa yote kuhakikisha kuwa watuhumiwa
wanachukuliwa hatua kali.
Tukio
la kuwaoza watoto katika umri mdogo siyo tu linakinzana na haki za
msingi za mtoto bali pia linamkosesha mtoto haki ya kuendelezwa ikiwa ni
pamoja na kuhatarisha uhai wake kwa kupatiwa majukumu ya mtu mzima
katika umri mdogo.
Wizara
inawataka wazazi na walezi kubadilika na kuachana na tabia ya kuwaoza
watoto wao katika umri mdogo maana vitendo hivyo ni vya kikatili. Jamii
inatakiwa kutambua kuwa, vitendo vya kikatili kama hivyo vinapofanywa
katika familia vinarudisha nyuma juhudi za Serikali za kupambana na
ukatili maana kwa kiasi kikubwa familia inatakiwa kuwa mahala salama
panapofaa watoto kuishi na kulindwa.
Aidha,
Wizara inakumbusha wazazi, walezi na wadau wengine kuwa, ndoa za
utotoni ni kinyume na Sheria ya Mtoto (2009) na Mikataba ya Kimataifa
kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto. NIwajibu wa kila mtu kuhakikisha kuwa
watoto wanaishi katika usalama na kuhakikishiwa haki zao zote za msingi
ikiwemo kulindwa, kuendelezwa, kuishi na kushirikishwa katika maisha ya
kila siku ili kujenga Taifa linaloheshimu maslahi ya watoto.
Erasto T. Ching’oro
Kny: KATIBU MKUU
Kny: KATIBU MKUU
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZAZI NA WATOTO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni