WAZIRI
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alitangaza kwamba anajiandaa
kugombea tena urais utakapofika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 2020.
Lowassa
alitangaza hayo mbele ya wafanyabiashara wa sokoni Kariakoo jijini Dar
es Salaam wanaojiita Team Mabadiliko, waliokwenda kumtembelea ofisini
kwake Mikocheni, Dar es Salaam.
Lowassa
alisema bado anazo nguvu na kumwezesha kugombea nafasi hiyo ya juu
kabisa katika uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hatua
hiyo inakuja wakati Lowassa akijipatia umaarufu zaidi kama mpambanaji
mahiri kisiasa, ambaye aliingia katika kinyang’anyiro hicho kwenye
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana, akisimamia kambi kuu ya upinzani
nchini.
Alijiunga
na upinzani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lakini
akapata kuungwa mkono na muungano wa UKAWA ulioundwa na chama hicho
pamoja na Civic United Front (CUF), National League for Democracy (NLD)
na NCCR-Mageuzi.
Ugombeaji
wake ulikuja baada uamuzi wake mgumu wa kuhama Chama Cha Mapinduzi
(CCM) alichoanzia siasa miaka ya 1980 hadi kufikia ngazi ya Waziri Mkuu,
wadhifa aliouteuliwa kushika Novemba 2005 hadi Februari 2008
alipojiuzulu kufuatia shinikizo la Bunge kutokana na kashfa ya mkataba
tata wa umeme wa Richmond.
Lowassa
alitoa ushindani mkali katika uchaguzi mkuu kiasi cha kuaminika kuwa
alipata kura za kutosha kutwaa urais, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ilimtangaza mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli kuwa mshindi.
Daktari huyo wa kemia aliapishwa rasmi Novemba 5, mwaka jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni