Rais
John Magufuli leo ameungana na wananchi katika kufanya usafi ambapo
akiwa katika eneo la Feri jijini Dar es Salaam, ameweza kuzungumza moja
kwa moja na wavuvi wadogo.
Baada
ya kusikiliza kwa makini kero zinazowakabili wavuvi hao wadogo akiwa
amekaa ndani ya kifaa duni cha kufanyia uvuvi maarufu kama ‘mtumbwi’
usio na mashine, rais Magufuli aliwaahidi wavuvi hao kuzitatua kero
hizo.
Kati
ya mambo matatu aliyoahidi kuyafanyia kazi kwa haraka ni pamoja na
kuondoa masharti kuwa kuwa na ‘Fire Extinguisher’ ambapo alieleza kuwa
sharti hilo halina mashiko kwa wavuvi hao wadogo wasio na mashine.
“Kwanza maji yenyewe tu ni ‘fire extinguisher’, si moto ukianza unaingia ndani ya maji,” alisema Dk. Magufuli.
Kadhalika,
rais aliahidi kuwasaidia wavuvi hao kwa masharti ya kuunda umoja wao
ambao utakuwa na viongozi waadilifu wanaofanya kazi kwa maslahi ya
wavuvi hao na sio maslahi ya ‘wakubwa’. Alieleza kuwa atalifanyia kazi
suala la wavuvi hao kukopesheka na kuwasaidia kuwa na vifaa bora.
Aliongeza kuwa atahakikisha anafuta ushuru kwa wavuvi hao wadogo ili kuwaondolea kero na mzigo wa gharama.
Pia, alisema atahakikisha anaanza kuwasaidia kadiri awezavyo wavuvi wa eneo la Feri kwa kuwa ni majirani zake.
“Katika kudhihirisha ujirani mwema, hayo matatizo nitayabeba.”
Hata hivyo, rais aliwataka wavuvi hao kuhakikisha hawajihusishi na uvuvi haramu wa kutumia sumu na mabomu.
Katika
hali ambayo wengi hawakuitegemea, rais Magufuli alimpa mmoja kati ya
wawakilishi wa wavuvi hao namba yake ya simu na yeye akachukua namba ya
watu wawili kati yao.
Akiongea
na waandishi wa habari baada ya zoezi hilo, Dk. Magufuli aliwashukuru
watanzania wote kwa ujumla kwa kuitikia wito wake wa kufanya usafi huku
akieleza kuwa hili linapaswa kuwa zoezi endelevu kwani uchafu hauwezi
kuisha kwa kufanya usafi mara moja kwa mwaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni