“Dunia imeharibika na binadamu hawana upendo wamegeuka kuwa na tabia kama za wanyama kila kukicha…” hiyo ni kauli yake Rehema Gwaya (41) mkazi wa Barabara ya Sokoine, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Rehema
ambaye ni mjasiriamali mdogo anayejishughulisha na kuuza juisi,
alipatwa na mkasa wa kumwagiwa mafuta ya moto ya kupikia ambayo yalikuwa
yanatumika kwa ajili ya kuchomea maandazi.
Inadaiwa
aliyefanya unyama huo ni mke wa shemeji yake baada ya kutokea
sintofahamu ya usafi wa mazingira ya nyumbani kwao, kama anavyojieleza:
“Tukio
limetokea mwishoni mwa Mei nikalazwa mwanzoni mwa Juni hadi sasa Julai
ambapo Daima Said (13) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Luseti
ninayeishi naye aligombana na mke wa shemeji yangu, Zefania Chimgege,
chanzo kikiwa ni suala la usafi wa mazingira kwani mama huyo alipaswa
kwenda kusafisha choo akakataa kukawa na mzozo mkubwa.
“Mzozo
huo ulitokea mimi nikiwa sipo, nilikuwa kwenye biashara zangu,
niliporudi nyumbani nilimfuata mama Chimgege ili anipe maelezo, ghafla
akanivamia na kuanza kunishambulia kwa maneno makali yaliyoambatana na
matusi.
“Wakati
huo mume wake alikuwa anachoma maandazi kwa ajili ya biashara yake,
wakati naendelea kutafakari kauli chafu alizozitoa dhidi yangu,
nilishitukia nikimwagiwa mafuta ya moto usoni, papo hapo nilianguka
chini jambo lililompa nafasi mama huyo kunikalia na kuanza kunichuna
ngozi iliyobabuka.
“Nilipoteza
fahamu na kujikuta nipo Hospitali ya Mkoa Songea, nimelazwa wodi ya
wanawake nikiwa na majeruhi usoni na kwenye matiti, hivyo naendelea
kupata matibabu.
“Nawaomba
Watanzania wenye mapenzi mema kunisaidia kwani kwa sasa siwezi kufanya
shughuli yoyote kutokana na kuuguza majeraha ya moto ambayo yana maumivu
makali na hapa nilipo nina mtoto mdogo wa miezi tisa ambaye ananyonya.
Kwa
upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea,
Dk. Benedikto Ngaiza amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo ambapo alisema
anaendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Mihayo Mikhela amekiri kutokea kwa
tukio hilo na amethibitisha kuwa mtuhumiwa anashikiliwa wakati upelelezi
unaendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni