Alhamisi, 2 Julai 2015

Wanne Wahukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa Baada Ya Kukutwa Na Hatia Ya Kumuua Albino


MKAZI wa Kiwira, wilayani Rungwe, Hakimu Mwakalinga ambaye aliwahi kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kukutwa na hatia ya kumuua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Rungwe, John Mwakenja, amehukumiwa adhabu hiyo kwa mara nyingine baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mlemavu wa ngozi (albino).
 
Mwakalinga pamoja na washitakiwa wenzake watatu walihukumiwa adhabu hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Henry Mwakajila (17) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino).
 
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa mahakama hiyo, Dk Mary Levira baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka kwamba washtakiwa hao walitenda kosa hilo.
 
Washitakiwa wengine ni Asangalwisye Kanyuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga ambaye ni mganga wa kienyeji, Gerad Kalonge na Leornda Mwakisole ambao ni wakazi wa Kiwira wilayani Rungwe.
 
Hata hivyo, mshitakiwa wa nne, Mawazo Figomole aliachiwa huru na mahakama hiyo baada ya ushahidi wa upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kuwa alihusika na mauaji hayo.
 
Kesi hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu namba KIW/IR/49/2008 na PI 5/2013 ni kesi ya saba ya mauaji ya albino kutolewa hukumu ambapo mpaka sasa jumla ya watuhumiwa 15 wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa.
 
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Februari 5, mwaka 2008 kati ya saa 12:00 na saa 1:00 jioni katika kijiji cha Ilolo, kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, washitakiwa hao walimteka kijana huyo ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Ukukwe na kumuua.
 
Wakati wa mwenendo wa kesi, ilidaiwa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwamba mshitakiwa wa kwanza Kayuni ambaye ni mganga wa jadi, alikutwa na utumbo unaodhaniwa kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitika kuwa ni utumbo wa marehemu Mwakajila.
 
Aidha, mshitakiwa wa pili Kalonge, alikutwa na vidole vinne na mifupa 10 vyote vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu na baada ya uchunguzi vilibainika kuwa ni viungo vya Mwakajila.
 
Ilidaiwa kuwa, washtakiwa Mwakisole, Figomole na Mwakalinga ndio walimteka nyara mtoto huyo na kumuua, kisha kupeleka viungo kwa mganga wa kienyeji.
 
Mwakalinga alihukumiwa Novemba, mwaka juzi baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Mwakenja ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo kwa kumpiga risasi.
 
Ilidaiwa kuwa Mwakalinga na wenzake watatu walifanya mauaji hayo kutokana na Mwakenja kufahamu kuwa wao ndiyo walimuua Mwakajila, hivyo walimuua ili kupoteza ushahidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa