Wakati joto la uchujaji wa majina ya wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likizidi kuongezeka, taarifa zimezidi kuzagaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii kwamba, mikakati ya kumuondoa Edward Lowassa kwenye orodha ya watia nia nayo imezidi kupamba moto.
Ofisa mmoja wa CCM makao makuu mjini
hapa, alisema kuwa wanachofanya wao kama watendaji ni kuandaa majina ya
wagombea wote na fomu zao za udhamini na kisha kukabidhi kwa
sekretarieti itakayopanga ajenda za vikao vya Kamati Kuu na baadaye
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya taifa.
Ofisa huyo alipoulizwa kama ana taarifa
za kuwako kwa mizengwe dhidi ya Lowassa alisema kwa ujumla kwa sasa kuna
maneno mengi sana yanazungumzwa juu ya mchakato wa uteuzi wa mgombea,
ila akasisitiza kuwa la msingi ni kusubiri vikao vya maamuzi.
“Ndugu yangu ukiyatazama haya makundi (ya urais) ni vigumu kuamini kama wanatoka chama kimoja. Yaani kuna kukamiana kweli kweli…Kila mmoja anataka kumwangusha mwenzake ili yeye apite,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hata
kama kuna mizengwe, si unajua uchaguzi huu ni wa vyama vingi. CCM
haishindani pekee yake, kwa hiyo mgombea anayekubalika ndiye anatakiwa.”
Hata hivyo, kwa muda sasa kumekuwa na
mfululizo wa habari za kupikwa kwamba jina la Lowassa litaishia Kamati
Kuu kwa madai kwamba kuna ushahidi wa matumizi ya fedha kwa timu yake,
tuhuma ambazo binafsi (Lowassa) amezikanusha mara kadhaa.
Julai mosi mwaka huu siku anarejesha
fomu za kuwania urais kupitia CCM alitoa changamoto kwa yeyote mwenye
ushahidi wa kuhusika kwake na rushwa ajitokeza na kusema alitoa lini,
wapi na kwa nani.
Lowassa alisema amechoka kwa tuhuma za
kipuuzi za kuhusishwa na rushwa na kusisitiza kuwa hakuna mwanachama
yeyote miongoni mwa zaidi ya nane waliomdhamini aliyefanya hivyo kwa
kishawishi cha fedha au fadhila yoyote.
Mgombea anayetajwa kutumiwa zaidi na kundi linalompinga Lowassa ni pamoja na Makongoro Nyerere, ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni na kuporomosha kauli kali za ukakasi dhidi ya Lowassa.
Wakati mizengwe ikizidi kusukwa dhidi ya
Lowassa, ripoti ya kura zote za maoni ambazo zimekuwa zikitolewa katika
miezi ya hivi karibuni zimeonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa mbali
kama chaguo la wananchi wengi kwenye nafasi hiyo.
Miongoni mwa tafiti hizo ni ule wa
Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, uliofanywa mwezi uliopita na matokeo yake kutolewa mwishoni
mwa wiki unaonyesha kuwa Lowassa ni changuo la kwanza la wengi kwa
kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho, huku Bernard Membe
akishikilia nafasi ya pili kwa kupata asilimia 8.2.
Katika utafiti huo ambao REDET walisema
kuwa unaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo
masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti,
wahojiwa walikuwa 1,250 kutoka wilaya moja moja katika mikoa 25 ya
Tanzania Bara.
Wakati mkakati wa mizengwe ukiendelea
kupamba moto, wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho
wanaanza vikao mjini Dodoma leo kundaa pamoja na mambo mengine ajenda na
taarifa kwenye vikao vya Kamati Kuu itakayokaa Alhamisi mjini hapa.
Kikao cha Kamati Kuu kinatarajiwa
kuchuka majina ya watia nia 38 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama
hicho na kubakisha majina matano tu yatakayopelekwa NEC kwa kupigiwa
kura.
NEC inayotarajiwa kukutana Ijumaa wiki
hii, itatoa majina matatu kwenda Mkutano Mkuu unaotarajiwa kukutana
Jumamosi kwa ajili ya kupata jina moja la mgombea urais wa CCM katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Mpekuzi blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni