Jumanne, 7 Julai 2015

LIPUMBA: Tutaitisha Maandamano Mikoa Yote Yenye GESI


Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kitaitisha maandamano kwenye mikoa yenye gesi ili kulishinikiza Bunge kupinga muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa juzi.
 
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na viunga vyake, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema haoni mantiki na hakuna sababu ya kufanya haraka kupitisha muswada huo.
 
“Suala hili linahitaji mjadala wa kina utaohusisha wadau mbali mbali, wataalamu na wananchi kwa ujumla wake,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
 
“CUF inaunga mkono jitihada za wabunge wa kambi ya upinzani kwa hatua zao kupinga muswada huo, ambao haukujali na wala haukuzingatia maslahi ya Taifa.”
 
Alisema CUF inatoa angalizo kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba kwa hali inavyoenda huenda akaenda kufunga Bunge litalokuwa na Wabunge wa CCM pekee.
 
“Hiyo inatokana na ukweli kwamba Spika wa Bunge amepoteza muelekeo na ameshindwa kabisa kuliongoza Bunge kwa mujibu wa kanuni walizojiwekea katika kutimiza wajibu,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
 
“Kwa hiyo  basi, Rais Kikwete atakuwa amefuata nyayo za Rais wa Zanzibar.”
 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein Juni 26, mwaka huu alilivunja Baraza la Wawakilishi bila Wawakilishi wa CUF kuwapo barazani.
 
Wajumbe hao walisusia Baraza hilo kutokana na kutoridhishwa na uandikishaji wa wapigakura katima daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama Biometric Voters Registrarion (BVR), wakisema kuwa uandikishaji huo ulitawaliwa na ubabe.
 
Profesa Lipumba alionya kuwa kama Bunge litaendelea na mpango wake huo, basi CUF  itaitisha maandamano ili kupinga muswada huo.
 
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema kuwa Mkoa wa Kigoma unaweza kuendelea kiuchumi ikiwa utatumia vizuri rasilimali zilizoko akitolea mfano Hifadhi ya Taifa ya Gombe kwamba ikitumika vizuri inaweza kuingiza mapato mengi.
 
Alisema kwamba jiografia ya Mkoa wa Kigoma inauruhusu kupata fursa nyingi za kuendelea kiuchumi kwa kuwa wananchi wake wanaweza kufanya biashara na nchi zinazouzunguka za Burundi Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa