CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimemfukuza uanachama Diwani wake wa Kata ya
Kasulu Mjini, Isack Rashid kikimtuhumu kutoa siri za chama na kuzusha
migogoro kati yake na viongozi wenzake.
Akitoa taarifa kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya
Kasulu, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, William Rutuli alisema kuwa
halmashauri imepokea barua kutoka chama hicho juu ya uamuzi huo.
Rutuli alisema kutokana na barua hiyo, diwani huyo anakosa sifa za
kuendelea kuwa mjumbe wa baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya
Kasulu na hivyo kata hiyo kwa sasa kuwa wazi.
Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo kumshukuru diwani huyo (hakuwepo
kwenye kikao) kwa kutumia muda wake wa karibu miaka minne na miezi
kadhaa katika kusimamia maendeleo kwa wananchi wa kata ya Kasulu mjini
na halmshauri hiyo kwa Jumla.
Akizungumza na mwandishi wetu, Diwani Rashid alikiri kupokea barua ya
kuvuliwa uanachama kutoka kwenye chama chake hivyo kupoteza nafasi yake
ya udiwani katika kata ya Kasulu mjini, ikiwa ni tuhuma tatu ambazo
zimesababishwa kuvuliwa uanachama.
Hata hivyo, Rashidi alisema mchakato mzima wa kumvua uanachama,
haukuwa halali kwani kikao maalumu cha Halmashauri kuu Zanzibar hakina
mamlaka ya kumvua uanachama, kwani kinafanya kazi zake upande wa
visiwani pekee.
Alisema kutokana na hali hiyo, amepinga kuvuliwa uanachama na kwamba
ameanza kufanya mchakato wa kupinga kisheria kuvuliwa uanachama kwa
kufuata taratibu na katiba ya chama hicho.
Kwa muda mrefu diwani huyo amekuwa kwenye mgogoro na Mbunge wa Kasulu
mjini, Moses Machali, hali iliyosababisha kuwa na mashitaka katika
ngazi mbalimbali za uongozi za chama hicho, kila mmoja akimtuhumu
mwenzake kuvuruga chama mkoani Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni