Bw. Mugusuhi Nyarusahe (39) aliyecharangwa kwa visu na wenzake.Stori:Gregory Nyankaira, Butiama/Risasi Mchanganyiko
MTU mmoja, Mugusuhi Nyarusahe (39) mkazi wa Kijiji cha Kinyambwiga
wilayani Bunda, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), cha
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara baada ya kucharangwa visu na wenzake
tumboni, katika kile kilichodaiwa kuwa ni mzozo wa mgawo wa fedha
zilizotokana na mauzo ya ng’ombe, tukio lililotokea wiki iliyopita.
Nyarusahe ambaye ni maarufu kwa jina la Serikali, alipatwa na mkasa huo
baada ya kuzuka ugomvi katika baa moja iitwayo Gateway Bar & Guest
House iliyopo Kiabakari wilayani Butiama.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kundi la watu sita lilifika katika
baa hiyo na kujitenga kando mishale ya saa 11 jioni na kuanza kuagiza
vinywaji huku wakiwa na mazungumzo yao.
Ghafla, watu hao walianza kumwagiana pombe ovyo vichwani na kuzua
taharuki kubwa kwa wateja wengine huku wakipasua chupa za bia na Mukebha
Marwa alichomoa kisu kutoka ndani ya koti alilokua amevaa na kumchoma
Mugusuhi na kusababisha utumbo kumwagika chini.
Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema watu hao walikuwa
wakibishana juu ya mgawo wa fedha zilizotokana na mauzo ya ng’ombe
wanaosadikika kuwa wa wizi.
Akizungumza akiwa hospitalini, Mugusuhi alisema ameanza kujitambua
baada ya kuzirai tangu alipochomwa kisu na kwamba baada ya kukatwa
utumbo mara tatu na kushonwa ameanza kupata nafuu “Mungu atanisaidia
nitapona,” alisema.
Jeshi la polisi kupitia kwa msemaji wake Kamanda ASP Alex Kalangi
limethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa hakuna mtu
aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni