Ijumaa, 6 Februari 2015

KUINGIA KWA SEKTA YA AFYA KATIKA BRN KUNALETA MATUMAINI MAPYA

Mtendaji Mkuu wa PDB Bw. Omari Issa akielezeaumuhimu wa sekta ya Afya kuingia BRN kuungana na sekta nyingine zilizotangulia zinazoendelea kuzaa matunda
kip2
Dr Linda Ezekiel ambae ni Mkurugenzi wa sekta za jamii (Afya, Elimu na Maji) PDB akiwasilisha mada kuhusu malengo ya kipaumbele sekta ya afya kwa miaka

kip3
Bw. Omari Issa akimkabidhi mwakilishi wa wahisani wa maendeleo mkakati wa sekta ya Afya chini ya BRN
kip4
Mmoja wa wahisani akisisitiza umuhimu wa wizara ya afya kuwajibika ki BRN katika maeneo mengine yasiyo ya kipaumbele katika BRN
kip5
Dr Oberline Kisanga wa kitengo cha mageuzi katika wizara ya afya akifafanua ushiriki wa TAMISEMI katika mkakati huu wa afya chini ya BRN
kip6
Mwakilishi wa jumuiya ya wahisani akipongeza uamuzi wa serikari kuiweka sekta ya afya katika BRN
…………………………………………………………………………………………
Annastazia Rugaba, PDB habari, 05 Februari 2015
Mtendaji mkuu wa Ofisi ya Rais, usimamizi wa utekelezaji wa miradi (PDB) Bwana Omari Issa, leo amekabidhi rasmi taarifa ya mkakati wa kuboresha sekta ya afya chini ya BRN kwa jumuia ya wahisani wa maendeleo. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za PDB ambapo jumuiya ya wahisani ilipata fursa ya kusikiliza kwa kina namna BRN inavyofanya kazi ya kuleta matumaini mapya kwa watanzania kupitia sekta za kipaumbele.
Sekta ya afya imekuwa ikijaribu kuboresha utendaji wake lakini kuingia katika BRN kutaleta tija Zaidi. BRN inaamini katika misingi mikuu ambayo ni kuweka vipaumbele, kuwa na adabu ya utekelezaji, uwajibikaji na uaminifu, ufuatiliaji wa kina na wa mara kwa mara na Mawasiliano thabiti kati ya watoa huduma na wapokea huduma. Hizi ni nguzo muhimu zitakazotufikisha katika dira ya maendeleo ya taifa ya Mwaka 2025.
Awamu ya kwanza ya BRN iliziangazia sekta sita ambazo ni Kilimo, Elimu, Maji, Uchukuzi, Nishati na ukusanyaji wa mapato ambapo sekta za Afya na Uboreshaji wa mazingira ya Biashara zimeanza rasmi Mwaka huu. Sekta sita za mwanzo zimedhihirisha mafanikio anuwai ambayo yaliwavutia jopo la wataalamu wa maendeleo wakiongozwa na Rais Mstaafu wa Botswana Bw Mogae. Ripoti kamili ya utekelezaji wa BRN kwa Mwaka wa kwanza itazinduliwa rasmi mapema mwezi Machi Mwaka huu.
Sekta ya afya inakusudia kutekeleza vipaumbele vine ambavyo ni mosi; ugawanyaji sawia wa wahudumu wa afya wenye ujuzi takikana kuanzia ngazi ya chini ya afya ya msingi, pili; utoaji huduma wenye ubora wa nyota tatu katika ngazi zote, tatu; upatikanaji wa dawa na bidhaa muhimu za afya katika ngazi zote, nne; kuimarisha afya ya uzazi na usalama wa mama na mtoto ili kupunguza vifo vya kundi hili muhimu kwa angalau asilimia 60 ifikapo Mwaka 2018.
Jumuiya ya wahisani wamepongeza uamuzi wa kuiingiza sekta ya afya katika BRN na wakithibisha utayari wao wa kufanikisha mkakati huu, wametoa wito kwa wizara ya afya, PDB, Sekta binafsi na jamii ya kitanzania kwa ujumla kuhakikisha kuwa mkakati huu utafanikiwa.
Malengo haya yote yanahitaji juhudi kubwa na ya pamoja kutoka kwa jamii, wizara na taasisi zake zote hadi ngazi ya kijiji, wahisani wa maendeleo na sekta binafsi. “tusingoje nani aanze, sote tuwajibike, kila mmoja ajitazame kama anawajibika ipasavyo. Dira ya maendeleo ya Taifa tunayotaka itupeleke kuwa nchi yenye uchumi wa kati haiwezi kufikiwa tusipofanya kazi kwa pamoja bila kunyoosheana vidole. BRN ni treni iliyoanza safari tayari, kila mmoja anawajibika kuingia kwa wakati na kwa nia Chanya, ukichelewa ukakuta imeondoka bado una fursa ya kuikimbilia kituo kinachofuata ili twende pamoja”Bw Omari Issa ametoa wito huo kwa wahisani wa maendeleo na jamii kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa