Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari katika
viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana.
Picha na Anthony Siame.
Dar/Dodoma. Licha ya Serikali
kusisitiza kuwa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima kwa mfumo wa BVR
utakamilika Aprili 28 na Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30, mwaka huu
kama ilivyopangwa, hesabu zilizopigwa na Mwananchi zinakataa kuwianisha
siku zilizosalia na idadi ya mashine za BVR zilizopo na zinazotarajiwa
kuwasili. Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimebaki siku 36 kabla ya Kura ya
Maoni kufanyika, huku kukiwapo wasiwasi miongoni mwa wadau kuhusu
uwezekano wa kufanikisha matukio hayo bila manung’uniko.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza waandishi wa
habari jana kuwa uandikishaji nchi nzima utaanza siku sita kuanzia leo
na kusisitiza kuwa Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba
Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Wasiwasi wa kutofanyika kwa kura hiyo katika
tarehe iliyopangwa unatokana na uandikishaji wa wapigakura kwa BVR
unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ulioanza Februari 23,
mwaka huu kutokamilika hata katika mkoa mmoja wa Njombe, wenye
wapigakura 392,634 kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini
kote.
Hesabu zinavyokataa
Kulingana na takwimu za NEC, BVR moja inaandikisha
kati ya wapigakura 80 hadi 100 kwa siku endapo hakuna tatizo lolote,
hivyo kwa kadirio la chini, iwapo BVR 7,750 zilizoagizwa na NEC
zitawasili nchini kwa mafungu, zitahitajika siku 38 kuandikisha
wapigakura milioni 24 wanaokusudiwa kama kazi hiyo itaanza leo.
Hata hivyo, katika uandikishaji wa majaribio na
baadaye katika Mkoa wa Njombe mashine hizo zimeripotiwa kukabiliwa na
changamoto mbalimbali ama za kukwama, weledi mdogo wa watumiaji na hali
ya hewa, hivyo kufanya idadi iliyokusudiwa kutokamilika.
Mwandishi wa Mwananchi, Kizzito Noya aliyekuwa
Makambako, Njombe wakati wa uandikishaji hivi karibuni amesema kwa
wastani alishuhudia mashine moja ya BVR ikiandikisha wapigakura 60 kwa
siku, idadi hiyo ikilinganishwa na watu 24,000,000 wanaokusudiwa
kuandikishwa kwa BVR 7,750 nchi nzima, shughuli hiyo itachukua siku 52,
wakati siku zilizosalia hadi Kura ya Maoni ni 36.
Jambo jingine linalofanya hesabu hizo kukataa ni
kitendo cha mashine hizo 7,750 za BVR zilizokusudiwa, kutokuwapo zote
nchini hadi sasa, licha ya NEC kusema mara kwa mara kwamba zitawasili
wakati wowote.
Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hata awamu ya kwanza ya mashine 3,100 za BVR bado ziko njiani.
Iwapo mashine hizo pekee zitafika na kutumika
kuandikisha wapigakura hao milioni 24 zitahitajika siku 97 kukamilisha
shughuli hiyo.
Mchakato huo ulianza kusuasua tangu wakati
majaribio yaliyotumia BVR 250 katika majimbo ya Kilombero, Morogoro;
Kawe, Dar es Salaam na Milele mkoani Katavi na baadaye katika Mji wa
Makambako na mkoa mzima wa Njombe.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa
mashine hizo 250 zimekuwa hazitumiki zote kwa kuwa baadhi zinatumika
kutoa mafunzo kwa waandikishaji watakaofanya kazi hiyo nchi nzima.
Changamoto nyingine inayokwamisha shughuli hiyo ni ukata, kwa
kuwa Serikali haijatoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo, jambo
ambalo limethibitishwa na Pinda kuwa fedha zilizotolewa hadi sasa ni
asilimia 70 ya kiwango kilichotarajiwa.
Kauli ya Lubuva
Jaji Lubuva alisema: “Tuliamua kuanza na Njombe
kutokana na BVR 250 tulizonazo kutosha katika mkoa huo wenye kata 99.
Tunasubiri nyingine 7,750 kuwasili wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi
ujao zikitokea China.”
Alisema uandikishaji Njombe unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika Aprili 12, kama ilivyopangwa.
Kuhusu uwezekano wa kura ya maoni kufanyika Aprili
30, alisema: “Kazi ya msingi kabla ya shughuli yoyote ni kuandikisha
daftari la wapigakura, hivyo kama tarehe itafika bado hatujamaliza
nitawaeleza, lakini mpaka sasa bado tarehe ya Aprili 30 haijabadilishwa.
“Vifaa 3,100 kati ya 7,750 viko njiani na
vitakapowasili tutatangaza ratiba, tutaanza na mikoa gani na Njombe
kweli wamehamasika kwani wamejitokeza kwa wingi na sisi kama tunaona
hatujamaliza licha ya ratiba kututaka kuhama tunaongeza siku ili
kuhakikisha kila mmoja anaandikishwa sasa mimi sielewi hao wanaosema
kwamba uandikishaji unakwenda sivyo hata huko bungeni sielewi wana
maanisha nini.”
Oktoba 22 mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete
alipokutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha
nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China, aliwaeleza kwamba kura hiyo
itafanyika Aprili mwaka huu.
Matumaini ya Pinda
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja
vya Bunge jana, Pinda alisema uandikishaji utaanza siku sita kuanzia leo
na Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba Inayopendekezwa itafanyika
Aprili 30, mwaka huu.
Alisema utoaji wa elimu kwa umma sambamba na
kampeni za kuiridhia au kuikataa Katiba hiyo, vinaweza kufanyika wakati
uandikishaji ukiendelea. Waziri Mkuu alisema Serikali imeshalipa
asilimia 70 ya fedha kwa kampuni inayosambaza mashine hizo.
“Tukianza uandikishaji nchi nzima ndiyo tutaona
changamoto zaidi zipo wapi na zinaweza kutupeleka katika uamuzi wa aina
gani. Ila hilo litakuwa jukumu la Tume (NEC), sisi kazi yetu ni
kuhangaika ili BVR zinazotakiwa ziwe zimepatikana kwa wakati,” alisema
Pinda.
Akizungumzia muda wa kampeni wa siku 30 kabla ya
Kura ya Maoni Pinda alisema: “Tume ndiyo inaweza kulizungumzia suala
hilo kiundani. Unajua inatakiwa mpaka kufikia Aprili 28 mambo yote yawe
yamekamilika na siku mbili baadaye (Aprili 30) ndiyo siku ya kura. Kama
wanasema mwezi mmoja ni sawa, tunaweza kuendelea na mambo mengine huku
elimu ikitolewa kwa wananchi.”
Alipoulizwa juu ya changamoto zilizojitokeza mkoani Njombe
alisema Serikali iliamua kuanza uandikishaji mkoani humo ili kupata
uzoefu kutokana na hali ya jiografia ya mkoa huo.
“Tulichojifunza ni kwamba katika maeneo ya
mijini, tukianza uandikishaji nchi nzima ni lazima maeneo kama hayo
tuyape nafasi kubwa zaidi tofauti na vijijini,” alisema.
Alisema maeneo ya mijini lazima mashine za BVR ziwe nyingi zaidi kuliko maeneo ya vijijini kwa sababu ya idadi ya watu.
Alisema katika Mkoa wa Njombe zilipelekwa mashine za BVR 250 lakini hazikutumika zote.
“Tumetenga siku saba kwa kila kata kwa ajili ya
uandikishaji nadhani zinatosha na kila kata tutaweka mashine za BVR
mbili hadi tatu,” alisema Waziri Mkuu.
Aliongeza: “Mashine hizo zinatosha kabisa. Kwa
uzoefu tulioupata pale Njombe hatuoni tatizo hata kidogo kwamba tunaweza
kushindwa kuandikisha wananchi na kutofikia malengo tuliyoweka.
Zinatosha kwa sababu leo wanaweza kuandikishia kituo kimoja na watu
wakiisha wanahamia kituo kingine. Kata ina vijiji vinne hadi vitano na
kila kijiji kina kitongoji kati ya vinne hadi vitano, hivyo muda wa siku
saba unatosha kabisa.”
Juzi, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
aliomba mwongozo bungeni akiitaka Serikali itoe majibu ya kueleweka juu
ya hatima ya uandikishaji wa wananchi katika daftari la Wapigakura
ulioanzia Mkoa wa Njombe na iwapo Kura ya Maoni itafanyika Aprili 30.
Alisema kuwa muda uliobaki ni ndoto kwa Serikali
kukamilisha uandikishaji huo nchini nzima, akitoa mfano kwamba ili
wananchi wa Mkoa wa Njombe waweze kuandikishwa wote, uandikishaji
unatakiwa kuongezwa muda hadi Aprili 28 na Spika alimjibu kuwa Serikali
ingetoa maelezo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni