Mtaalam
kutoka Kampuni ya Sweco International AB, Pal Aberg (kushoto)
akiielezea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini hatua
iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro
kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiendelea na ziara katika eneo
la kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo Njiro nje kidogo ya
jiji la Arusha.
Mtaalam
kutoka Kampuni ya Sweco International AB, Pal Aberg (kulia) akitoa
maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye
eneo la kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro kilichopo nje
kidogo ya jiji la Arusha.
Wataalam
kutoka kampuni ya Sweco International AB, wakiendelea na ujenzi katika
kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro kilichopo nje kidogo ya
jiji la Arusha.
Mtaalam
kutoka Kampuni ya Sweco International AB, Pal Aberg (kushoto) akitoa
maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye
chumba cha kuendesha mitambo ya umeme ( control room) ndani ya kituo cha
kupooza na kusambaza umeme kilichopo Njiro nje kidogo ya jiji la
Arusha.
Meneja
Mradi katika Kituo cha Kupooza na Kusambaza Umeme cha KIA Mhandisi
Emmanuel Manirabona (kulia) akiielezea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo hicho kilichopo
mkoani Kilimanjaro
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa (wa
kumi na moja kutoka kushoto), Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco), Felchesmi Mramba (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na
wajumbe wa kamati hiyo na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini
mara baada ya kukamilisha ziara yake katika kituo cha kupooza na
kusambaza umeme cha KIA kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Mjumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa
Viti Maalum Jimbo la Singida, Martha Mlata (kushoto) akisalimiana na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
Dkt. Miganda Manyahi (kulia), jijini Arusha kabla ya kuanza kwa ziara
kwenye miradi ya umeme. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
inafanya ziara katika miradi ya umeme iliyopo katika mikoa ya Arusha na
Kilimanjaro ili kujionea hatua ya utekelezwaji wake pamoja na kuzungumza
na watendaji.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Richard Ndassa
(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Felix Ntibenda
(kulia) mara baada ya Kamati hiyo kuwasili ofisini kwake kwa ajili ya
kupokea taarifa ya mkoa kabla ya kuanza kwa ziara kwenye miradi ya
umeme.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Daudi Felix Ntibenda ( wa nne kutoka kushoto
waliosimama mbele), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini Richard Ndassa ( wa tano kutoka kushoto waliosimama mbele)
wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini mara
baada ya kumalizika kwa kikao.
Meneja
Mradi wa Kusambaza Umeme unaojulikana kwa jina la Electricity V
unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi Florence
Gwang’ombe (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini Richard Ndassa (kulia) mara baada ya kamati
hiyo kuwasili kwenye eneo la mradi huo ili kujionea maendeleo ya
utekelezwaji wake.
- Ni baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa bilioni 72.5
- Wateja wapya 30,000 kuunganishwa
Na Greyson Mwase, Arusha
Meneja
Mradi wa Kusambaza Umeme unaojulikana kwa jina la Electricity V
unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi Florence
Gwang’ombe amesema kuwa tatizo la kukatika katika kwa umeme katika
mkoa wa Arusha litakwisha mapema Juni mara baada ya kukamilika kwa
kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo katika eneo la Njiro,
nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mhandisi
Gwang’ombe aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini iliyofanya ziara katika kituo hicho ili kujionea
maendeleo yake pamoja na kuishauri serikali jinsi ya usimamizi wake.
Alisema
mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho mbali na kuboresha
upatikanaji wa nishati ya umeme katika jiji la Arusha, wateja wapya
wapatao 30,000 wanategemewa kuunganishiwa umeme kutoka katika kituo
hicho.
Akielezea
mradi huo kwa ujumla Mhandisi Gwang’ombe alisema kuwa mradi huo
unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa mkopo wa
kiasi cha shilingi za kitanzania 72,588, 506,400 unahusisha ujenzi wa
njia za umeme wenye urefu wa kilomita 480 za msongo wa kilovoti 33 na
ufungaji wa transfoma 102 za kusambaza umeme zenye ukubwa wa 33/0.4 kV.
Alisema
pia mradi huu unahusisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya kupoozea
umeme vya Ilala, Sokoine katika mkoa wa Dar es Salaam na upanuzi wa
kituo cha kupoozea umeme cha Njiro.
Alisisitiza
kuwa mradi unatekelezwa na Mkandarasi National Contracting Company
ambaye alishinda zabuni ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kupoozea
umeme katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha na mkandarasi Eltel
Networks TE AB ambaye alishinda zabuni ya ujenzi na ukarabati wa mifumo
ya kusambazia umeme katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
Akielezea
hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Njiro,
Mhandisi Gwang’ombe alisema kazi zinazoendelea katika kituo hicho ni
pamoja na ufungaji wa transfoma mbili na ufungaji wa mitambo ya kisasa
kwa ajili ya kuendesha na kulinda mifumo ya umeme.
Aliongeza
kuwa uagizaji na utengenezaji wa vifaa umekamilika kwa asilimia 85,
kazi za ujenzi zimekamilika kwa asilimia 76 pamoja na kumalizika kwa
kufunga na kuunganisha vifaa na mifumo ya umeme.
Alisisitiza
kuwa mradi huu unategemewa kuongeza ukuaji wa uchumi katika mkoa wa
Arusha pamoja na mikoa mingine kama Shinyanga na Mwanza kwani
utachochea ukuaji wa viwanda vidogo vidogo na biashara katika maeneo
husika pamoja na kuongeza fursa za ajilra kwa wananchi.
Aliendelea
kusema kuwa mradi huo utaboresha huduma za jamii kwa wananchi kutokana
na upatikanaji wa umeme mashuleni, mahospitalini na kwenye maeneo
mengine ya jamii husika na hivyo kupunguza umasikini kwa wananchi
jambo ambalo linaendana na malengo ya siasa ya nchi.
Akizungumzia
lengo la mradi, Mhandisi Gwang’ombe alisema kuwa lengo la mradi ni
kuongeza uwezo wa kusambaza umeme wenye kiwango kinachotakiwa na
usiokatikakatika na kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
kuweza kuwafikia na kuwapatia umeme wenye uhakika wateja wengi zaidi
ambao bado hawajapatiwa huduma ya umeme.
Wakati
huo huo, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Mhandisi
Felchesmi Mramba aliiambia Kamati ya Bunge kuwa ongezeko la wateja wa
kawaida na viwanda lilisababisha ongezeko la kasi la matumizi kufikia
Megawati 70 hali iliyopelekea shirika kuboresha na kujenga vituo
vya kupoozea na kusambazia umeme.
Mhandisi
Mramba alisema, kabla ya ujenzi wa kituo hicho, hali ya umeme katika
jiji la Arusha ilikuwa ni mbaya hali iliyopelekea ujenzi wa kituo hicho
na kusisitiza kuwa Shirika limeamua kufanya mapinduzi katika sekta ya
umeme kwa kuhakikisha linashirikiana na wawekezaji mbalimbali na
wataalamu wake katika ujenzi wa vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme
ili kuzalisha nishati ya umeme ya uhakika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni