Jumatano, 11 Machi 2015

HOFU YA UFISADI YAMFANYA WAZIRI WA UCHUKUZI KUZUIA UINGIZAJI MABEHEWA 124 YA MIZIGO YA KAMPUNI YA RELI TANZANIA.


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta


Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amezuia uingizaji wa mabehewa 124 ya mizigo yaliyobaki katika zabuni iliyofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), hadi pale uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika manunuzi hayo utakapokamilika.



Pamoja na hayo, Sitta alisema kuna hisia zimejitokeza kuwa huenda mabehewa hayo ni mitumba siyo mapya kama inavyodhaniwa.


Sitta aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa zabuni ilihusisha ununuzi wa mabehewa 274 na kwamba 150 tayari yalishaingia nchini, huku kukiwa na harufu ya ufisadi kuwa yalitengenezwa chini ya kiwango.


Mapema Aprili 2013, TRL iliipatia kampuni ya India iitwayo M/S Hindustan Engineering & Industrial Limited zabuni ya kutengenezea mabehewa ya mizigo kwa ajili ya Reli ya Kati. Serikali iliilipa kampuni hiyo Sh45.5 bilioni sawa na Sh166 milioni kwa kila behewa.


Hata hivyo, Sitta alisema kuwa Serikali ililipa asilimia 50 ya gharama zote za manunuzi na kwamba iwapo ikibainika udanganyifu wowote kampuni hiyo itawajibika.


“Nimekataza kabisa yale 124 yaliyobaki kule yasije. Nimeshawaagiza Reli kuwa yaliyopo kiwandani yanaendelea kutengenezwa au safarini hayaruhusiwi kuja kwa sasa mpaka tuweze kukwamua sakata hili.”


“Haiwezekani wakati tunachunguza 150 yaliyoingia tukayaruhusu yale 124 yaingie. Je, yakiwa na ubovu ule ule itakuwaje?” alihoji Sitta.


Alisema anaungana na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa mabehewa hayo ya mizigo yapo chini ya kiwango kutokana na kupinduka na kuacha reli mara kwa mara.


Alisema kiwango cha kuacha reli kwa mabehewa hayo siyo cha kawaida na ripoti ya Desemba mwaka jana ilionyesha kulikuwa na wastani wa upindukaji kila siku.


Kutokana na suala hilo kuwa kikwazo cha ufanisi kwa TRL, Sitta aliiagiza kamati ya uchunguzi wa sakata hilo (iliyoundwa na Dk Mwakyembe) kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kukamilisha ripoti ifikapo Ijumaa wiki hii ili Serikali ijue la kufanya.


“Kuna mambo mengi tu ya kufanya kama kuvunja mkataba na mkandarasi, kumshtaki mhusika, kuangalia nani walienda kukagua na bado tukapata vibovu.


“Hii itatusaidia kujua hatua za kuchukua kiuwajibikaji kwa kuwa hivi sasa ni lazima mtu awajibike aidha kwa kufanya jambo kwa makusudi au kwa uzembe,”alisema Sitta. Alisema Idara ya Uhandisi katika wizara yake itasaidia kubaini nini kilitokea kiasi cha kuingiza nchini mabehewa yanayoleta hasara kubwa kwa taifa.


Kuhusu utendaji wa jumla wa TRL, Sitta alisema kwa sasa hali inaridhisha katika kampuni hiyo kiasi cha kuongeza mapato maradufu hadi kufikia Dola za Marekani 140 milioni (Sh252 bil) Desemba, 2014 kutoka Dola 38 milioni (Sh68.4 bil) Januari mwaka huo.


Alisema mabehewa mapya ya abiria yanatarajia kuanza kufanya kazi Aprili baada ya kukamilisha taratibu za Sumatra huku akibainisha kuwa hadi Julai mwaka huu watakuwa na vichwa 60 dhidi ya 107 vinavyohitajika.MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa