Jumamosi, 31 Januari 2015

Chenge Ageuka Mbogo Bungeni baada ya kuitwa FISADI.......Amtaka Halima Mdee Atoe Ushahidi Kuthibitisha Kauli yake



MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) ametakiwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha kauli yake ya kumtuhumu Mbunge Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), kwa ufisadi.
 
Chenge alilazimika kuomba utaratibu wa kiti JANA, baada ya Mbunge huyo wa Kawe kumtaja mara mbili wakati akichangia mjadala wa taarifa za kudumu za Bunge zilizowasilishwa jANA.
 
Mara ya kwanza, Mdee alimhusisha Chenge na mkataba mbovu wa Kampuni ya Ndege (ATCL) uliosababisha Serikali kuingia hasara ya zaidi ya Sh bilioni 90.
 
Licha ya kumtaja kwenye ufisadi huo ambao kwa mujibu wa Mdee, Chenge ndiye alikuwa Waziri wa Wizara yenye dhamana na ATCL, pia alimtaja kuhusika katika kashfa nyinginezo ikiwemo suala la utoaji takribani Sh bilioni 200, katika iliyokuwa Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu (BoT).
 
“Wabunge tuanze kuchunguzana humu ndani na kushughulikiana,” alisema Mdee na kutaja kwamba kwa kuanza, waanze na Chenge pamoja na Dk Shukuru Kawambwa (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi), akimhusisha kuwa aliwahi kushika wizara hiyo yenye dhamana na ATCL.
 
Kauli hiyo ilimfanya Chenge kusimama na kusema; “kwa heshima zote nimemvumilia sana mheshimiwa (Mdee) anayechangia hoja hii. Kama ana ushahidi wa hayo anayosema, kanuni zetu zinatutaka ayawasilishe mbele yako.
 
“Mimi ningelipenda Bunge hili liendelee kuwa na heshima yake. Pili naomba sana, hayo wanayoyasema wawe na ujasiri wa kwenda kuyasemea nje ya ukumbi huu wa Bunge, wasijifiche kwenye kinga ya Bunge.
 
 “Nina mengi ya kusema, lakini kwa sababu nimesimama kwa hoja ya utaratibu, kunitaja moja kwa moja, naomba aweke hoja mezani,” alisema Chenge.
 
Mwenyekiti wa Bunge alikubaliana kwamba Mdee awasilishe ushahidi kwa kiti. Hata hivyo Mdee alijibu, “Kuna utaratibu wa kikanuni, vielelezo nikitakiwa kuleta nitaleta.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa