Jumapili, 25 Januari 2015

Kung'oka kwa Pofesa Muhongo ni hitimisho la matukio mengi tangu Waziri huyo aanze kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.


Sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow linaweza kuwa limefanya jina la Profesa Sospeter Muhongo kuzungumzwa sana na kuonekana amekuwa kwenye wakati mgumu tangu lilipoibuka, lakini ukweli ni kwamba lilikuwa hitimisho tu la matukio mengi tangu msomi huyo aanze kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.
 
Muhongo, ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge Mei 3, 2012 kabla ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri, amekuwa kwenye kiti moto wakati wote tangu ashike uwaziri kutokana na kashfa ambazo hazikomi kwenye sekta ya madini na nishati, na tabia yake ya kushambulia wanaotoa hoja kwa maneno ya dhihaka na kujisifu, ambayo mara nyingi yalikera watoa hoja.
 
Mikataba 26
Waziri Muhongo alianza kazi kwa kuliagiza Shirika la Mafuta (TPDC) kupitia upya mikataba 26 ya utafutaji gesi, hatua ambayo iliungwa mkono na wengi huku wakitaka ripoti ya kazi hiyo iwe bayana ili Watanzania wajue uozo uliopo, hata hivyo, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi huo, Profesa Muhongo hakuweka bayana matokeo ya ripoti hiyo, badala yake akasema ripoti hiyo itatumika wakati wa kuingia mikataba mipya tofauti na alivyoeleza mwanzo kuwa angefuta mikataba mibovu.
 
Akajikuta anaingia kwenye mzozo na wadau, hasa wabunge, na miaka miwili baadaye, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ikaiagiza menejimenti ya TPDC kupeleka mikataba hiyo kwenye kamati, lakini menejimenti ikagoma, kitendo kilichosababisha viongozi wa shirika hilo wakamatwe.
 
Kampuni ya Puma Energy
Hatua iliyozua tafrani zaidi ni ile ya wizara yake kuipa kampuni ya Puma Energy zabuni ya ugavi wa mafuta mazito kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa, hasa bungeni ambako watunga sheria walidai kuwa zabuni hiyo ilitolewa bila ya kufuata Sheria ya Manunuzi. Wabunge walidai kuwa Puma Energy haikuwemo kati ya kampuni zilizoomba, na kutuhumu kuwa kulikuwa na rushwa.
 
Wabunge walitaka Profesa Muhongo na katibu wake, Eliackim Maswi wawajibishwe, hoja iliyosababisha mgawanyiko mkubwa bungeni kiasi cha CCM kuitisha kikao cha wabunge wake kupanga mikakati ya kumuokoa waziri huyo.
 
Katika sakata hilo, Profesa Muhongo aliingia kwenye mgogoro na mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye alichangia hoja. Katika majibu yake, Profesa Muhongo alisema kuwa alikuwa akidhani mbunge huyo kuwa ni msomi, na akalazimika kufuatilia elimu yake. 
 
Alipotaka kueleza matokeo ya kidato cha nne ya Ole Sendeka, Spika Anne Makinda alimzuia na kumtaka aendelee na hoja iliyokuwa mbele yake.
 
Wafanyabiashara wazawa
Tabia ya Profesa Muhongo kujibu hoja kwa kushambulia walioitoa iliamsha mjadala mkubwa baada ya wafanyabiashara wakubwa kulalamika kuwa wizara hiyo haitoi kipaumbele kwa wazawa katika utoaji wa leseni za utafutaji gesi na mafuta. Katika kujibu hoja hiyo, mtaalamu huyo wa jiolojia, aliwaita wafanyabiashara hao kuwa ni madalali na hawana uwezo wa kufanya kazi hiyo.
 
Alieleza kuwa kazi hiyo inahitaji mtaji mkubwa. Alisema maombi tu ya kazi hiyo yanagharimu Dola 700,000, wakati takwimu za kazi hiyo zinagharimu Dola 3 milioni, utafutaji Dola 15,000 hadi 20,000 kwa mita moja ya mraba, kuchoronga kwenye kina kirefu kuna gharimu Dola 1 milioni kwa siku, wakati kumaliza tundu moja ni Dola 1 na yanahitajika matundu 12.


Pia alisema kuchimba kwa ajili ya kupitisha mabomba kwenda nchi kavu kunagharimu dola 200. Profesa alisema hayo bungeni huku akitamba kwamba yeye ni msomi na wabunge wanaojaribu kujenga hoja hizo ni mawakala ambao “wana-retire imprest” kwa kuzungumza bungeni, akimaanisha kuwa wanaonyesha kwa waliowalipa fedha kuwa wametekeleza kazi waliyotumwa.
 
Kufuta leseni za vitalu
Pia alizua kizaazaa kingine aliposema kuwa atapitia leseni zote za vitalu vya madini na kufuta vile ambazo hazifanyi kazi kama sheria inavyotaka. Alisema kuna leseni 597, lakini wanaolipa kodi ni wanaomiliki vitalu 10 tu na baadaye akatangaza kuwa alishafuta leseni za vitalu zaidi ya 150 na alikuwa anakusudia kufuta nyingine 78.
 
Mkakati wake uliwagusa wafanyabiashara wengi wazawa na mara kadhaa walipokutana walitoa kauli ya kulaani misimamo ya mbunge huyo wa kuteuliwa.
 
Wakati kashfa ya escrow ilipoanza, Profesa Muhongo alitumia tena mbinu yake ya kushambulia watoa hoja kwa kueleza kuwa maneno hayo yote yanatokana na uamuzi wake wa kufuta mkataba wa Tanesco na kampuni ya uwakili ya Mkono, akisema ililipwa Sh62 bilioni na hivyo kuwa moja ya taasisi zinazotafuna fedha za shirika hilo la umma.
 
Katika kashfa ya escrow, Profesa Muhongo anatuhumiwa kwa kushindwa kushughulikia vizuri sakata hilo la uchotwaji fedha kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa kwa pamoja na Tanesco na IPTL baada ya pande hizo mbili kuingia kwenye mgogoro na kufungua kesi mahakamani.
 
Akitoa utetezi wa Serikali bungeni, Profesa Muhongo alitumia staili yake ya kuwananga waliokuwa wakituhumu huku akijisifu kuwa ni msomi. Alieleza kuwa fedha hizo, Sh306 bilioni, hazikuwa mali ya umma bali za IPTL, lakini hoja zake zikapingwa vikali na wabunge ambao walionyesha nyaraka mbalimbali kuthibitisha kuwa msomi huyo hakusema ukweli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa