Jumamosi, 31 Januari 2015

MKASA MZIMA WA YULE MAMA ALIYEWANYONGA WATOTO WAKE WAWILI WA KUWAZAA KWA UCHUNGU NA KUWAFUKIA NDANI KWAKE:

BADO hali ni tete kufuatia mwanamke mmoja, Zuhura Sudi (26), mkazi wa Mtaa wa Utusi Kata ya Chemchemi Manispaa ya Tabora kudaiwa kuwaua kwa kuwakaba shingo watoto wake wawili, Mwamvua (6) na Sudi Mrisho (miezi saba) kisha kuwazika kwenye mashimo mawili ndani ya nyumba.

Mwanamke (Zuhura Sudi) anayetuhumiwa kuwaua watoto wake.
Tukio hilo ambalo limeishangaza nchi hasa kufanywa na mama mzazi ambaye anaujua uchungu wa kuzaa, lilijiri Jumapili usiku ndani ya nyumba ya mwanamke huyo.
SIKU MOJA KABLA
Taarifa kutoka vyanzo vya uhakika, siku moja kabla ya tukio, mwanamke huyo ambaye ni mtata kiasili alionekana akicheza na watoto wake na watoto wa jirani huku akionesha uchangamfu mkubwa.
“Kama wale watoto wake wangejua mama yao mzazi ndiyo safari ya kifo chao naamini wasingemchangamkia mama yao.
“Walicheza kwa amani, kwa upendo. Kumbe mama ana mahesabu yake. Haiwezekani leo niambiwe kuwa mawazo ya kuwaua watoto wake aliyapata ghafla,” alisema shuhuda mmoja.
Mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi.
USIKU, JIRANI ASIKIA KISHINDO
Jirani mmoja na nyumba ilipotokea tukio alisema:
“Mimi awali ya siku ya kuelekea usiku wa tukio, nilimwona yule mama. Nikasalimiana naye. Alionekana yupo kawaida tu.
“Lakini usiku, kukiwa kumetulia nilisikia vishindo kama mtu anachimba ardhi. Nilipofuatilia nikabaini vilikuwa vikitoka upande wa nyumbani kwa mwanamke yule.“Sikushtuka. Nilijua ni shughuli zake za  kawaida zinaendelea ndani ya nyumba yake. Kulipokucha sasa, nikasikia yule mama anasema kwamba watoto wake wamepotea.
“Palepale nikaanza kuhisi kitu kwa ile mishindo ya usiku. Inaonekana alishawaua watoto wake sasa alikuwa anachimba mashimo ya kuwafukia. Kule si kuwazika na yale si makaburi ni mashimo. 
“Inauma sana, siamini kama mama aliyezaa watoto kwa uchungu mkubwa anaweza kufanya ukatili kama huu.”
Miili ya watoto hao baada ya kufukuliwa kwenye mashimo.
AKILI ILIMWAMBIA ASUBIRI AKIWA PEKE YAKE
Baadhi ya majirani walisema ndani ya nyumba hiyo kuna watu wengine wanaishi, lakini mtuhumiwa huyo alisubiri akiwa peke yake ndipo akatekeleza ukatili wake wa kutisha.
ANACHOJUA MWENYEKITI WA MTAA
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Utusi, Aziza  Mwenya, ushirikiano mkubwa  kati ya  wananchi  wa mtaa  huo  ndiyo uliofanikisha  kugundulika  kwa tukio  hilo  la  kinyama  lililopoteza  maisha  ya  watoto  hao  wasiokuwa na hatia.
“Baada  ya  kupokea taarifa  kutoka  kwa  babu  wa  Zuhura, mzee Shaban Ramadhan kuhusu  kutoweka  kwa watoto  hao katika  mazingira ya kutatanisha, tulifika  kwenye nyumba ya tukio kwanza na kumhoji  mama wa watoto.
Ndugu na majirani wakiwa na makamanda wa Polisi eneo la tukio.
“Cha ajabu  alikuwa akizuia watu  kuingia ndani. Kumbe alishajua kinachoendelea na akiruhusu sisi kuingia nini kitatokea.“Hata hivyo majirani kwa kushirikiana na mimi na baba wa mmoja wa watoto waliouawa (Sudi Mrisho), Mrisho Abdallah tulimshika kwa nguvu  Zuhura, watu wakaingia.”
WAKUTA MASHIMO MAWILI
“Tulipofika, tukabaini mashimo mawili aliyokuwa amewafukia watoto wake. Shimo moja sebuleni, jingine chumbani. Tuliwapa taarifa polisi wakafika haraka sana. Mashimo yalipofukuliwa, watoto walikutwa ndani ya mifuko miwli ya sandarusi. Inauma sana. ”
MTUHUMIWA AZUNGUMZA NA AMANI
Amani lilibahatika kuzungumza na mwanamke huyo katika mahojiano mafupi akiwa chumbani muda mfupi kabla ya polisi kufika.Amani: “Hivi Zuhura, ni kwanini umeamua kuwaua watoto wako wa kuwazaa?”
Zuhura: “Nani? Mimi sijui, we (mwandishi) ndiyo unajua.”Amani: “Watoto wako wako wapi?”
Zuhura: “Nani? Wako wapi kwani?”
KILICHOONEKANA
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema, Zuhura licha ya kuonekana hana wasiwasi wowote, lakini pia aliashiria kujitoa ufahamu ili atafsirike kwamba hakuwa na akili timamu.
KUMBUKUMBU MBAYA
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa majirani zinadai kuwa, mwaka 2013, Zuhura alidaiwa kumsababishia kifo mtoto wake mchanga  wa kiume kufuatia kumzidishia dozi ya malaria wakati alipokuwa akiumwa.
KAMANDA WA POLISI
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,  ACP Juma Bwire ilikiri kutokea kwa tukio hilo.
Afande Bwire alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa