SERIKALI
inakusudia kutumia Sh bilioni nane katika mpango wake wa kulipanga upya
Jiji la Mwanza kwa kuainisha sehemu za makazi, viwanda, biashara na
huduma za kijamii.
Kauli
hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Mpango Mkakati
wa Kuyapanga Majiji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Mahenge Amulike, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau na
viongozi wa Serikali wa sekta zote wa kupokea maoni na mapendekezo ya
kuainisha maeneo hayo.
Pia
aliwataka wakazi wa Mwanza na Arusha kutambua hakuna haja ya kumiliki
eneo kubwa la ardhi kwa ajili ya kujenga nyumba nyingi badala yake
wanapaswa kumiliki eneo dogo ili kujenga ghorofa.
Alisema
Serikali imeamua kuainisha maeneo ya majiji hayo kwa sababu ya ardhi
kutoongezeka huku watu wakiongezeka kwa kasi hivyo ni lazima maeneo
yakapangwa katika utaratibu unaotakiwa ikiwa ni kuepusha majanga
yanatokana na watu kuishi katika maeneo hatarishi bila wao kujua.
Alisema
tatizo kubwa lilipo kwa Watanzania ni kutaka kumiliki eneo kubwa la
kujenga nyumba kitendo kinachosabisha watu wengine kukosa ardhi na
kukosekana sehemu ya kuweka huduma za kijamii.
“Watu
wanaongezeka kwa kasi lakini ardhi ipo pale pale tena mahitaji
yanaongezeka, sasa bila kuyapanga majiji hayo kutakuwa na hatari
mbeleni, lazima ardhi igawanywe kwa utaratibu unaokubalika, ni vema
umiliki viwanja viwili kwa kujenga ghorofa 10 hadi 20 kuliko kumiliki
ardhi kubwa na kujenga nyumba nyingi.
“Wapo
watu wanaoishi milimani na mabondeni hao wapo hatarini, chukulia
asilimia 70 ya wakazi wa Mwanza wanaishi milimani palipo na mawe, sasa
jiwe la asili halitakiwi kuguswa au kuchimbwa lakini watu wamejenga
nyumba juu ya mawe, ndiyo maana tunasikia yanaporomoka na hao maisha yao
yapo hatarini,” alisema Amulike.
Alisema
Serikali ya Tanzania ilisaini mkataba Januari 15 mwaka huu na watalaamu
wa mipango miji kutoka Singapore ili kuyapanga majiji ya Arusha na
Mwanza na ndani ya miezi 19 watashughulikia kuainisha na kupanga maeneo
hayo.
Alisema baada ya kazi ya kuainisha kukamilika utaanza kutekelezwa na utakuwa na mkataba mwingine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni