WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la
ugonjwa wa malaria kwa kuamua kujenga kiwanda cha kisasa cha kutengeneza
dawa za kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha ugonjwa huo.
Kiwanda
hicho cha viua wadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ungonjwa wa
malaria, kimejengwa eneo la Tamco wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza
baada ya kukagua kiwanda hicho juzi, alisema ana imani kujengwa kwa
kiwanda hicho kutamaliza tatizo la malaria hapa nchini na katika nchi za
jirani.
“Malaria
ni ugonjwa hatari na unaongoza kwa kusababisha vifo hapa nchini. Watu
karibu milioni mbili wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa
huu. Tukianza kutengeneza hizi dawa zitasaidia kupunguza tatizo hili na
kuokoa maisha ya watoto na wajawazito ambao ndiyo waathirika wakubwa.
“Dawa
hizi zinapotumiwa katika madimbwi, viluwiluwi ni lazima watakufa katika
muda wa saa 24 na katika dimbwi hilo dawa ile inabaki ikifanya kazi
kwa muda wa mwaka mmoja.
"Hii ina maana wakizaliwa viluwiluwi wengine pia wanakufa bila hata kuweka dawa nyingine,” alisema Pinda.
Kiwanda
hicho kitakachotoa ajira za moja kwa moja 186, kinatarajiwa kuzinduliwa
Juni 25, mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete na kinatarajiwa kuanza
uzalishaji wa majaribio mapema mwezi ujao.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, aliwaomba Watanzania kujenga viwanda vingi zaidi katika mkoa huo.
Akitoa
maelezo kuhusu utengenezaji wa dawa hizo wakati Pinda akikagua kiwanda
hicho, Msimamizi Mkuu wa Ujenzi, Dk. Ricardo Menendez, alisema ujenzi wa
kiwanda hicho hapa nchini utatoa fursa kwa Tanzania kuuza dawa hizo kwa
nchi za Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambazo pia
zinasumbuliwa na tatizo la malaria.
“Tukishazalisha
dawa za kutosha na kuzisambaza mikoa yote, itabidi tuangalie uzalishaji
wa kibiashara kwa ajili ya nchi jirani zenye tatizo kama hili, hiki ni
kiwanda pekee barani Afrika,” alisema Menendez.
Kiwanda
hicho kinachojengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la
Maendeleo (NDC) na Kampuni ya Labiofamsa ya Cuba, kitakuwa na uwezo wa
kuzalisha lita milioni sita za dawa ya ‘biolarvicides’ kwa mwaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni