HUKUMU
ya kesi inayowakabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba,
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na wenzao inatarajiwa
kusomwa Juni 30, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Uamuzi
huo ulifikiwa jana mbele ya jopo la mahakimu watatu likiongozwa na Jaji
John Utamwa baada ya kupangwa kwa tarehe za majumuisho ya mwisho wa
kesi hiyo. Mahakimu wengine katika kesi hiyo ni Sam Rumanyika na Saul
Kinemela.
Mbali
na Mramba na Yona, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo iliyochukua
takriban miaka saba ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Uchumi, Gray Mgonja.
Washitakiwa
hao wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na
kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kutokana na kutoa
msamaha wa kodi kwa kampuni iliyopata zabuni ya ukaguzi wa madini ya
dhahabu nchini ya M/S Alex Stewart.
Upande
wa utetezi na ule wa Jamhuri umepangiwa tarehe za kuwasilisha
majumuisho yao ya mwisho iwapo wanaona washitakiwa wana hatia au la,
baada ya kukabidhiwa mwenendo wa kesi hiyo Jumatatu, wiki ijayo ambapo
utakuwa umeshakamilika kuchapwa.
Mahakama
hiyo iliuamuru upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao Juni 9, mwaka huu
na upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu ya hoja za utetezi Juni 17,
mwaka huu, huku upande wa utetezi iwapo utakuwa na majibu ya nyongeza
kuwasilisha kabla ya Juni 25, mwaka huu na hukumu itatolewa Juni 30,
mwaka huu.
Wakati
wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa Jamhuri uliita mahakamani
hapo, mashahidi saba na baada ya kufunga ushahidi wao, washitakiwa
walionekana wana kesi ya kujibu hivyo kutakiwa kutoa utetezi wao.
Kwa upande wa utetezi, walitoa ushahidi wao wenyewe wakiwa na mashahidi wao wawili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni