JOTO la ubunge kwenye jimbo la Arusha Mjini, limezidi kupanda mara baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha, Francis Laizer kutangaza rasmi kuwania ubunge katika jimbo hilo, endapo akipewa ridhaa na chama chake kugombea.
Laizer amejitokeza kutangaza azma hiyo ikiwa ni siku chache baada ya
makada wengine wa CCM, ambao ni Phillemon Mollel, Victor Njau,Thomas
Munisi, Deo Mtui, Kim Fute kutangaza nia ya kuwania jimbo hilo
linaloshikiliwa na mbunge wake, Godbless Lema(Chadema) ambaye tayari
ametangaza kugombea tena.
Akizungumza na Mtandao huu jijini hapa, Laizer alisema amesukumwa na
dhamira ya kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya kuwepo kwa
changamoto nyingi, ambazo zimekosa mbunge wa kuzitatua kwa kipindi cha
miaka mitano.
Alisema amefanya utafiti wa kina na kubaini changamoto lukuki
zinazolikabili jiji la Arusha, ambazo zimeshindwa kutatuliwa na hivyo
kuona ana uwezo mkubwa wa kufanya mabadiliko na kuwaletea wananchi wake
maendeleo.
Kada huyo alisisitiza kwamba miongoni mwa mambo ambayo atakwenda
kuyafanyia kazi, pindi akifanikiwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo ni
kushughulikia changamoto kubwa ya ajira kwa vijana na kinamama na wazee
wa jimbo la Arusha Mjini.
Alitaja masuala mengine ambayo atatoa kipaumbele ni usalama wa raia
na mali zao, kwani limekuwa ni tatizo kubwa kiasi cha kuharibu heshima
na sifa ya jiji kwa matukio ya maandamano ya mara kwa mara yasiyokuwa na
tija kwa maendeleo ya jiji.
Alisema kuwa Arusha ni mji wa kimataifa na kuwa umekuwa ukikabiliwa
na changamoto ambazo zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa kutosha, kwani
matukio hayo yameharibu biashara ya utalii wa ndani na kupunguza ujio wa
watalii kutoka nchi za kigeni na kupunguza mapato kwa jiji la Arusha na
serikali kwa ujumla.
Hatahivyo, alibainisha kuwa atashughulikia changamoto nyingine ambazo
zimedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi zikiwemo za maji safi na
salama, ujenzi wa shule za sekondari za kidato cha tano na sita kwa
kata zote ili kuondokana na changamoto ya wanafunzi wanaofaulu kukaa
majumbani kutokana na ukosefu wa madarasa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni