KAMBI
Rasmi ya Upinzani bungeni, jana imeibua tuhuma nzito bungeni Mjini
Dodoma dhidi ya Kampuni ya Simu nchini (TTCL), ikidai aliyekuwa Meneja
Biashara wa kampuni hiyo (bila kutajwa jina), amefungua akaunti nchini
yenye kiasi cha sh. bilioni moja.
Waziri
Kivuli wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. Habib Mnyaa (CUF),
aliyasema hayo wakati akisoma hotuba ya kambi ya upinzani kuhusu
makadirio, matumizi ya fedha kwa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa, tuhuma
hizo ni kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Alisema
ubadhirifu wa fedha kwenye taasisi mbalimbali za Serikali imeota mizizi
ambapo baadhi ya watumishi wameamua kujilipa mafao ya kustaafu na
kujiongezea mikataba ya ajira.
Aliongeza
kuwa, vitendo vya aina hiyo ndio vinavyoendelea katika kampuni ya TTCL
vikipata baraka za Wizara husika ambapo baadhi ya watumishi wake
wanajinufaisha.
"Mbali
ya ufisadi huu, iweje hisa asilimia 35 za Serikali zilizopo ndani ya
TTCL zikodishwe kwa Kampuni ya Mobile System International (MSI) kwa
kulipiwa sh. bilioni 111 sawa na hisa asilimia 17 lakini Serikali
imewapa kuongoza kampuni na hawakulipa pesa yoyote," alihoji.
Bw.
Mnyaa alisema hisa zinauzwa na kununuliwa lakini cha ajabu,
zimekodishwa kwa anayedaiwa kuwa mwekezaji jambo ambalo ni maajabu kwa
tasnia nzima ya uchumi na uhasibu.
Aliongeza
kuwa, Kamati ya Wafanyakazi wa TTCL iliandika barua kwa CAG aweze
kwenda kufanya ukaguzi maalumu na kuandika barua nyingine kwa Ofisi ya
Bunge kuelezea hujuma zinavyofanywa na watendaji waandamizi wa kampuni.
"Ndani
ya TTCL kuna umiliki wa SEACOM lakini licha ya Serikali kulijua hilo,
bado wanailipa MSI sh. bilioni 14.9, tunamtaka Waziri mwenye dhamana
atoe majibu na maelezo ya kutosha juu ya suala hili," alisema Bw. Mnyaa.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wameitaka Serikali kuhakikisha kampuni za simu za mkononi haziwaibii wananchi.
Wakichangia
bajeti ya Wizara hiyo, wabunge hao walitaka kujua kama sheria za
mitandao ya simu zinabadilika kila mwaka wakidai baadhi ya kampuni za
simu zinawaibia wateja wao ambao wengi wao ni maskini jambo ambalo
halikubaliki.
Akichangia
hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, mkoani Mara, Ester Midimu (CCM),
alisema inashangaza kuona baadhi ya kampuni hizo zinawakata fedha wateja
wao hata kama hawajajiunga na huduma wanazotoa.
"Tulikuwa
tunanunua baadhi ya vifurushi kwa sh. 2,800 na kupata dakika zaidi ya
100 lakini hivi sasa tunapata dakika 80, swali langu kila mwaka sheria
zinabadilika au la?" Alihoji.
Mbunge
wa Chalinze, mkoani Pwani, Bw. Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema hivi
sasa baadhi ya kampuni hizo zinawaibia wananchi na kusisitiza kuwa, wizi
huo ni mkubwa.
"Tunataka ufafanuzi mzuri juu ya hili kwani ukiweka fedha katika simu inaisha haraka, huu ni wizi mkubwa," alisema.
Kwa
upande wake, akiwasilisha makadirio ya bajeti yake, Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, aliliomba
Bunge lipitishe sh. bilioni 66.9 kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni