WAKATI ugawaji wa majimbo 211 ukikamilika kwa vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), imebainika kwamba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibuka na asilimia 50 katika majimbo hayo.
Chama
kilichofuata ni Chama Cha Wananchi (CUF) ambacho kinadaiwa kupata
asilimia 35-40, NCCR-Mageuzi asilimia 10 huku NRD kinachoongozwa na
Emmanuel Makaidi kuachiwa asilimia 1-2.
Taarifa
ambazo MPEKUZI imedozwa zinadai kuwa mgawanyo huo umefanywa kwa
kuzingatia vigezo vya nguvu za kila chama katika eneo husika.
“Ndiyo
maana umeona huu mchakato umechukua muda mrefu kwasababu ilikuwa
inafanyika tathimini kuona nani ana nguvu wapi na nani ana nguvu eneo
gani mwisho wa siku umeona kwa haya 211 wamekubalina,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe.
Akizungumzia majimbo 12 yaliyoleta utata anasema “Majimbo haya ni sita ya hapa Dar es Salaam ambayo kuna Segerea, Temeke, Ukonga, Ilala na Kinondoni.
“Kwa
mikoani kuna jimbo la Serengeti, hili linaleta utata kwasababu kuna
mvutano kati ya watu wa Chadema na katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi Mosena
Nyambabe ambaye analitaka lile jimbo.
“Lakini
taarifa zilizopo ni kwamba Nyambabe aliangukia pua katika uchaguzi wa
serikali za mtaa na Chadema waliibuka kidedea, sasa ameambiwa kuachia
jimbo lakini yeye hataki, ndiyo na lenyewe limewekwa kiporo.
Taarifa
hizo zinaendelea kudai kuwa jimbo jingine lililotea mgogoro ni Vunjo
linaloshikiliwa na TLP ambapo tayari Mwenyekiti wa NCCR-James Mbatia
tayari ameonyesha nia ya kugombea.
“Huku
nako kuna mgogoro mwingine kwasababu tayari Mbatia ameshatangaza nia na
amefanya kazi kubwa katika jimbo hilo, lakini kuna kada mkubwa wa
Chadema aliyewahi kugombea jimbo hilo naye ameweka msimamo kwamba ni
lazima agombee."
Majimbo
mengine yanayotajwa kuweka umoja huo njia panda ni pamoja na Mtwara
mjini na Mafia ambapo taarifa kutoka kwa kiongozi mmoja wa Ukawa
zinasema kuwa wamepeana siku kumi kuanzia leo (jana) kwa kila kiongozi
kuhakikisha amekamilisha mchakato wa kukamilisha utaratibu kwa majimbo
yaliyobaki.
Katika
makubaliano Jimbo la Vunjo liliachwa mikononi mwa NCCR-Mageuzi ambapo
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia amejinadi kulichukua kutoka
mikononi mwa mbunge wa sasa Agustino Mrema.
Akizungumzia Makaidi kupewa asilimia moja mpaka mbili alisema kuwa inatokana na mzee huyo kuonyesha msimamo ndani ya umoja huo.
“Makaidi
hakuonyesha tamaa kama viongozi wengine wa upinzani baada ya kususia
kwenye Bunge la Katiba, hakuonyesha tamaa ya kutaka posho za Bunge la
Katiba, aliweka msimamo hadi leo hii, kwahiyo ndani ya Ukawa Mzee
Makaidi ameonekana shujaa."
Wadadisi
wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa Chadema ndiyo chama chenye nguvu
ndani ya Ukawa ambapo taarifa za ndani zilidai kuwa katika mchakato wa
kugawana majimbo kulikuwa na mvutano mkali huku chama hicho kikitaka
kuachiwa majimbo mengi hali iliyobua mgogoro kutoka katika vyama
vingine.
Lakini
duru za kisiasa zinaendelea kuonyesha kuwa mgawanyo huo pia unaweza
usieleweke kwa wanachama wa kawaida wa Chadema wakiwemo wabunge wao
ambao wanashikilia majimbo mbalimbali.
MPEKUZI
imepata mawasiliano ya kundi moja la wabunge wa Chadema wanalolitumia
katika mtandao wa kijamiii likionyesha kushangazwa na baadhi ya vyama
kutaka majimbo wanayoyashikilia.
Wabunge
walioshiriki mjadala huo walionyeshwa kushangazwa na kitendo cha CUF
kuomba kuachiwa baadhi ya majimbo wanayoyashikilia huku wengine
wakionyesha shaka kwamba inawezekana ni njia ya chama hicho kutaka
kuvunja umoja huo.
Katika
kuonyesha kukasirishwa mmoja wa wabunge alikwenda mbali zaidi na kutoa
angalizo kwa viongozi wao wa juu kuacha kuwaendekeza CUF huku mwingine
akipendekeza chama hicho kuwaachia Chadema majimbo ya Zanzibar.
Mbunge huyo aliyataja majimbo ya Zanzibar ambayo wangependa waachie kuwa ni pamoja na Pemba na mji mkongwe.
Mwingine
aliyechangia katika majadala huo alisema CUF wana undugu na CCM isije
ikawa wametumwa kuubomoa Ukawa, huku mwingine akichangia kwa kusema kama
ni mkakati wa kuingia Ikulu kwa upinzani ni sawa lakini kama siyo hivyo
kuna sababu za kubishana kulinda majimbo yao.
Majimbo
yaliyotajwa kumezewa mate na wabunge hao ni Musoma Mjini,Nyamagana na
majimbo mengine mengi huku mmoja wa wabunge waliokuwa wakishiriki
mjadala katika kundi hilo alisema kwa muktadha huo Ukawa ni shiidaa huku
mwingine akisema ni matusi kwa CUF kutaka majimbo yao.
MPEKUZI
ilipata wakati mgumu wa kuwapata viongozi hao wa Ukawa kwani hata wale
waliofikiwa wamekataa kuzungumzia jambo hilo huku taarifa zikidai kuwa
wamepeana onyo kali katika vikao vyao kuhakikisha hakuna anayetoa
taarifa za vikao nje.
Katika
mkutano wa Juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema Ukawa
iko imara sasa kuliko kipindi cha nyuma na alikanusha chama chake
kuandika barua ya kujiondoa katika umoja huo.
Ukawa ni muungano wa vyama vinne vya upinzani ambapo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NRD.
Muunganiko
huo ulifanyika katika Bunge la Katiba ambapo lengo lake kugomea Katiba
Pendekezwa wakiamini wanaburuzwa na chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo
baadaye waliamua kuendeleza umoja huo katika mambo mengine ya Urais.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni