DIWANI
wa Kata ya Ngula wilayani Kwimba, Palu Mashagu (CUF), anashikiliwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kuomba
na kupokea rushwa ya Sh 150,000.
Taarifa
kutoka Kwimba na kuthibitishwa jana na Kamanda wa Takukuru, Faustine
Maijo, ilisema Mashagu alikamatwa Mei 6, mwaka huu mchana katika ofisi
ya Mtendaji wa Kata ya Ngula akidaiwa kuomba na kupokea Sh 150,000
kutoka kwa mtumishi wa Halmashauri ya Kwimba, Nyabugumba Jonathan.
Mashagu
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kwimba anadaiwa kuomba na
kupokea kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumsaidia mtumishi huyo
pamoja na wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu
wa Sh milioni 72 za mradi wa usafi na mazingira.
Kutokana
na tuhuma hizo kufika katika vikao vya Halmashauri ya Kwimba, kikao cha
Baraza la Madiwani kiliazimia kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na
kuunda kamati ya madiwani watano chini ya uenyekiti wa Diwani wa
Nkalalo, Enos Ntwale, kuchunguza wizi wa fedha hizo kabla ya hatua
nyingine dhidi ya wahusika kuchukuliwa.
Wajumbe
wengine wa kamati hiyo ni Shija Malando (Kata ya Hungumalwa), Peter
Msalaba (Kata ya Nyambiti), Tabu Samson (Viti Maalumu) na Mashagu.
Akizungumzia
taarifa za diwani wake kutiwa mbaroni kwa kosa la rushwa, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Kwimba, Zephania Masangu, alisema amepokea taarifa hizo
lakini hajui undani wake na kubainisha alikuwa miongoni mwa wajumbe wa
kamati yake aliyounda Aprili 29, mwaka huu.
“Kamati
niliyounda ilishakamilisha kazi yake na taarifa kukabidhiwa sasa
maelezo zaidi nadhani wanajua waliomkamata mngewauliza wao,” alisema Masangu.
Akizungumzia
suala hilo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyekataa jina lake
kuandikwa alidai taarifa walizopokea katika kamati yao zimedai Mashagu
aliomba rushwa ya Sh 500,000 kwa Ofisa Afya Msaidizi aliyetoa taarifa
Takukuru ndipo ukawekwa mtego na kumnasa akipokea Sh 150,000.
Mpekuzi blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni