Jumamosi, 30 Mei 2015

Mbunge Ahoji ziara ya Obama Nchini


MBUNGE wa Viti Maalum, Amina Abdallah Amour (CUF) ameitaka Serikali kueleza imefaidikaje na ujio wa Rais wa Marekani, Barrack Obama mwaka 2013.
 
 Akiuliza swali bungeni jana, Mbunge huyo alisema mwaka 2013 Tanzania ilipata ugeni huo wa Rais wa Marekani na kutaka kujua faida za kisiasa na kiuchumi kutokana na ujio huo.
 
 “Je Taifa limefaidika vipi kisiasa na kiuchumi kutokana na ujio wa kiongozi huyo mkubwa duniani?” alihoji.
 
 Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mahadhi Juma Maalim alisema akiwa Tanzania Obama alitangaza mpango wa Serikali yake wa kusadia miradi ya umeme ujulikanao kama Power Initiative.
 
 “Kupitia mpango huo, Serikali ya Marekani imetenga Dola za Marekani bilioni 7 wakati wa sekta binafsi nchini Marekani imetenga Dola bilioni 9,” alisema.
 
 Alisema pia  katika kupambana na ujangili, Serikali ya Marekani imetoa vifaa vya mafunzo na mafunzo ya kujenga uwezo wa wataalamu.
 
 “Machi 2015, Marekani ilitoa msaada wa vitabu milioni 2.5 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5.
 
 “Kupatikana kwa vitabu hivyo kumesaidia kupunguza uhaba wa vitabu vya masomo ya sayansi na kupunguza uwiano wa upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi,” alisema.
 
 Alisema ziara za viongozi wakuu wa nchi ni njia mojawapo muhimu ya kukuza urafiki na uhusiano baina ya Tanzania na nchi nyingine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa