Bilia Masanja Mhalala.
Abubakar Ally Magazi.
Elizabeth au Shija Makandi Sweya na Regina au Tatu Kashinje Nhende.
Muhoja John Shija.
**************
**************
WATU sita, akiwemo Mwalimu wa Shule ya Msingi Katunguru iliyoko Kata
ya Wendele, Tarafa ya Msalala wilayani Kahama, wamekamatwa mjini hapa
wakiwa na vipande sita vya mifupa inayodhaniwa kuwa ya albino.
Taarifa zilizopatikana mjini hapa zimeeleza kwamba, mwalimu huyo
Bahati Kilungu Maziku (56), Msukuma na mkazi wa Mtaa wa Mbulu katika
Halmashauri ya Mji wa Kahama, amekamatwa akiwa na watu watano, wakiwemo
waganga wa jadi watatu, katika harakati za kuuziana mifupa hiyo.
Wengine waliokamatwa ni mganga wa jadi Bi. Elizabeth au Shija Makandi
Sweya (42), mkazi wa Busongwahala, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora,
Bilia Masanja Mhalala (39), Msukuma, mkulima na mkazi wa Mogwa wilayani
Nzega, mke wa Biria ambaye ni mganga wa jadi Regina au Tatu Kashinje
Nhende (40), Msukuma na mkazi wa Mogwa.
Aidha, watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Muhoja John Shija (24),
Mnyamwezi na mkazi wa Isagenhe wilayani Nzega pamoja na mganga wa jadi
na mfanyabiashara Abubakar Ally Magazi (25), Mrundi na mkazi wa Nzega.
Taarifa za uchunguzi wa awali zinaeleza kwamba, Mwalimu Bahati ndiye
aliyesuka mpango mzima akishirikiana na waganga wa jadi Bi. Shija
Makandi ambaye ndiye aliyeitafuta mifupa hiyo na Abubakar Magazi ambaye
alikuwa apelekewe ili ‘kuibetua’ (kuitengeneza) na kuzalisha fedha.
Watuhumiwa watano wanadaiwa kwamba walifunga safari kutoka Nzega hadi
Kahama kwa Mwalimu Bahati, ambaye kwa mujibu wa maelezo ya awali, ndiye
aliyejua ni wapi ambako mifupa hiyo ingeuzwa, hivyo walikuwa wanakutana
hapo kwa ajili ya kugawana fedha.
Mifupa hiyo inadawa kuhusishwa na tukio la kukatwa mkono wa kulia Bi.
Muungu Masaga Gedi (35) mwenye albinism, mkazi wa Kitongoji cha
Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata ya Igoweko wilayani Igunga, ambalo
lilitokea Mei 16, 2014 na kufunguliwa Jalada Namba IGU/IR/1070/2014.
Katika tukio hilo, mume wa majeruhi huyo, Mapambo Mashili, aliuawa
kwa kukatwa mapanga na watu wasiofahamika wakati akipambana na watu hao
wasimdhuru mkewe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP Justus Kamugisha,
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 21, 2015 na kwamba watu hao
walikamatwa saa 7:00 mchana katika nyumba moja ya kulala wageni
inayofahamika kwa jina la Maji Hoteli iliyopo Phantom, Kata ya
Nyasubi mjini Kahama baada ya Polisi kuweka mtego kufuatia taarifa za
wasamaria wema.
Taarifa ya Kamanda Kamugisha imesema kwamba, mnamo Mei 19, asubuhi,
mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Nzega alipata taarifa kuwa kuna mtu
anauza viungo vya albino, ndipo walipoweka mtego. Hata hivyo, alisemai
kuwa walishindwa kuwakamata na baadaye mtu huyo alihamishia biashara
hiyo wilayani Kahama.
Hata hivyo, jeshi la polisi bado linaendelea na msako dhidi ya watu
wengine wanaotajwa kwamba ndio walioitafuta mifupa hiyo, na kwa mujibu
wa taarifa za awali, ndio waliohusika na mauaji pamoja na kumjeruhi mama
huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni