UMOJA
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeridhia Chama cha Wananchi (CUF)
kusimamisha wagombea wake wa nafasi ya ubunge katika majimbo yote ya
uchaguzi visiwani Zanzibar, isipokuwa katika Jimbo la Kikwajuni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Makao Makuu ya CUF, Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Sheikh, alisema Ukawa
wamekubaliana katika Jimbo la Kikwajuni watasimamisha mgombea ubunge
kutoka Chadema ambaye ni Salum Mwalimu.
Mwalimu ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), ambaye hata hivyo tangu ateuliwe amekuwa akifanya kazi zake Tanzania Bara.
Jimbo
la Kikwajuni linaunganisha wakazi wa maeneo ya Kikwajuni Juu na Chini,
Kisimamajongoo, Kilimani, Miembeni, Magereza na sehemu ya eneo la
Michenzani.
Uamuzi
wa Mwalimu kusimama kuwania ubunge Jimbo la Kikwajuni kupitia Chadema,
umepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa siasa ndani ya
jimbo hilo huku wakionesha uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30
huenda utaleta changamoto kubwa kwa CCM.
Changamoto
kubwa inayoonekana kwa CCM ni kwamba, Mwalimu amezaliwa na anatoka
katika familia yenye makazi katika eneo maarufu la Kisimamajongoo ambalo
lilikuwa ni kitovu cha harakati za siasa za Chama cha Afro Shiraz
(ASP).
Wachambuzi
wanasema kwa namna moja ama nyingine familia ya Mwalimu nayo ilishiriki
kinagaubaga katika harakati za kudai ukombozi kwa Mzanzibari
zilizofanywa na hayati Mzee Karume.
Eneo
la Kisimamajongoo ndilo lilikuwa kitovu cha harakati za ASP kudai uhuru
wa Mzanzibari kutoka kwa Sultani na Wanamapinduzi walikuwa wakikutana
katika eneo hilo kupanga mikakati yao wakiongozwa na hayati Mzee Karume
katika nyumba yake aliyoipa jina la ‘Ndiyo’.
Hata hivyo, zilipokuja siasa za ushindani, baadhi ya wakazi wake wakagawanyika na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).
Wakazi
wa eneo la Kisimamajongoo wanaaminika ni ndugu wa damu na hilo ndilo
linasemwa huenda likawa ni moja ya jambo litakalowavutia wananchi wa
jimbo hilo kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuamua kumpa uongozi
Mwalimu wakiamini ni kijana wao na hatowaangusha.
Mwalimu
licha ya kuwa amezaliwa katika eneo la Kisimamajongoo, lakini
wachambuzi wanasema pia katika uchaguzi huo atabebwa sana na umaarufu wa
mama yake mzazi ambaye ni mtangazaji maarufu nchini, Faudhiyat Ismail
Aboud.
Kwa
sasa Jimbo la Kikwajuni kwa nafasi ya ubunge linaongozwa na Hamad
Yussuf Massauni (CCM), ambaye pia ni mzaliwa wa eneo la Kisimamajongoo
na hata katika uchaguzi wa mwaka 2010 alibebwa na turufu hiyo.
Inaaminika
katika uchaguzi huo wananchi wote wa Jimbo la Kikwajuni kwa pamoja
wakiongozwa na kampeni zilizofanywa na wakazi wa eneo la Kisimamajongoo,
waliamua kumpa kura Hamad wakiamini kuwa ni kijana wao.
Wachambuzi
wanasema uamuzi wa Ukawa kumsimamisha Salum Mwalimu, umefanywa
kiutafiti zaidi wakiamini utaamsha ushindani mkubwa katika jimbo hilo
ambalo limekuwa chini ya mikono ya CCM miaka yote.
Katika
hatua nyingine, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya, anatarajiwa
kusimama tena kutetea nafasi yake katika uchaguzi ujao akichuana na
Mwanahabari Maarufu, Ally Saleh ambaye ameshatangaza nia.
Katika nafasi ya Uwakilishi, CUF imemteua Ismail Jussa Ladhu kuwania nafasi hiyo akiwa ndiye mgombea pekee kutoka chama hicho.
Wakati
huo huo, Mwandishi wetu kutoka Zanzibar, Is-haka Omar, anaripoti kuwa,
CUF Zanzibar kimeeleza kuwa hatua yake ya kuendelea na mchakato wa
uchaguzi ndani ya chama hicho katika majimbo 49 ya Zanzibar haiendi
kinyume na makubaliano ya umoja huo.
Chama
hicho kimesema hatua hiyo haitaathiri makubaliano kati ya vyama hivyo
ya kuachiana majimbo katika uchaguzi mkuu ujao baada ya umoja huo
kuridhia chama hicho kusimamisha wagombea katika nafasi zote za
uchaguzi.
Pia
CUF imesema jumla ya wanachama 327 wa chama hicho wamepitishwa kuomba
kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge na uwakilishi wa majimbo na katika
viti maalumu vya wanawake Zanzibar.
Kati
ya wanachama hao, 133 wameteuliwa kugombea ubunge, 134 uwakilishi
katika majimbo 49 huku wengine 29 wameteuliwa kugombea ubunge kupitia
viti maalumu sawa na wengine 30 walioteuliwa kugombea uwakilishi.
Wagombea
hao watapigiwa kura na wajumbe wa mikutano mikuu ya majimbo na wilaya
ili kupatikana kwa mgombea mmoja ambaye ataidhinishwa na kikao cha
baraza kuu la chama hicho.
Katika
hatua nyingine chama hicho kimeendelea kusisitiza kuitaka ofisi ya
vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi kuwapatia wananchi vitambulisho hivyo
kabla ya kuanza kwa uandikishaji wa duru la mwisho unaotarajiwa kuanza
wiki ijayo katika Jimbo la Micheweni ili kuepuka vurugu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni