Jumatano, 27 Mei 2015

Nyota Ya Lowassa Bado Inang'aa: Utafiti Mpya Waonyesha Anaongoza Kwa Kupendwa na Wapiga Kura Wengi......Wafuatia Slaa, Magufuli na Membe


Nyota ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, imeendelea kung’aa baada ya Taasisi ya Samunge Social Sciences Research Center (SSSRC), kufanya utafiti na kubaini kuwa kiongozi huyo ni chaguo la kwanza kwa wananchi.

Utafiti huo uliofanywa miaka miwili kuanzia 2013 hadi 2015, unaonyesha Lowassa anaongoza kwa asilimia 20.7 dhidi  ya wagombea 31.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtafiti Mkuu wa SSSRC, George Nyaronga, alisema utafiti huo waliufanya kwa kutumia madodoso pamoja na mahojiano kwenye mikoa 18.

Utafiti huo na asilimia walizopata wanasiasa wengine kwenye mabano ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema, Dk. Willbrod Slaa asilimia 11.7; Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (7.6); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (7); Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (4.8); Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (4.2)  na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 3.4 sawa na Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (2.4) na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia (1.2).

Alisema pia utafiti huo ulionyesha kuwa Lowassa pekee ndiye anayekubalika na wapiga kura wengi, karibia idadi sawa ya jinsia zote mbili, wanaume 50 na wanawake 49.

Kwa ujumla, Lowassa na vinara wengine 10 wanaotajwa kuwania urais walipata asilimia 67.2, huku asilimia zilizobaki (32.8) zikitwaliwa na wagombea wengine 10 kati ya 20 waliohusishwa katika utafiti huo.

Aidha, Nyaronga alisema hawakuwa na dodoso  linaloorodhesha majina ya wanaopendekezwa kuwa Rais ila majina yalitajwa na wajaza madodoso wenyewe kisha wao wakajaza majina kwenye SSSRC.

Kwa mujibu wa dodoso lenye kichwa cha habari cha katika tafiti kuhusu uchaguzi wa mwaka 2015, takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania wanamtaka mtu mwenye kufanya maamuzi magumu.

Alisema kwa maoni ya wengi waliohojiwa na kujaza dodoso, wanaonyesha kuwa Lowassa anakubalika zaidi na kwamba ulifanywa katika mikoa 18 ya Bara na Visiwani, watu 1,000 walijaza dodoso na 6,000 walifanyawa mahojiano.

Alisema utafiti huo uliofanywa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Morogoro, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Katavi, Kigoma, Tabora, Arusha, Moshi, Iringa, Njombe, Songea, Lindi na Mtwara .

Nyaronga alisema baadhi ya mambo ambayo tafiti hiyo ilikuwa ikitafuta majibu ni masuala yanayohusu changamoto kwa Tanzania kwa sasa, sifa za kiongozi anayehitajika kukabiliana na changamoto hizo, mapendekezo ya jina la Rais atakayesimamia vizuri changamoto hizo, chama chenye uwezo wa kutupatia rais ajaye kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977 na kama Watanzania watapiga kura.

Vyama  vya  Siasa
Alisema utafiti huo umebaini CCM ina asilimia 53.5 ya kutoa Rais , Chadema yenye asilimia 34.2.

Alisema  vijana wa miaka kati ya 18-25 ambao ni sawa na asilimia 46 wanamtaka Lowassa kuwa Rais, ikifuatiwa na vijana wa miaka 26-30, na  vijana wa kati ya miaka 30-35.

Aliongeza kuwa CCM kina wanachama wengi wenye umri mdogo ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa Tanzania na Chadema ndicho kinachofuatia kwa kupendwa na umri wa miaka kati ya 18 -25.

Mtafiti huyo alisema CCM inapendwa zaidi na watu wenye aina mbalimbali za elimu kuanzia shahada ina watu 144, sekondari ina watu 84  na hata katika elimu ya msingi ina watu 18, ikifuatiwa na Chadema.

Alizitaja changamoto kuu 16 zilizopo Tanzania kwa sasa kama zilivyoorodheshwa na wananchi ambapo wanamtaka Rais ajaye azishugulikie ni elimu, afya, viwanda, ajira, kilimo, miundombinu hafifu, kukosekana kwa utawala bora, uchumi hafifu, nishati, migogoro ya ardhi, mikataba mibovu.

Nyingine ni ukwepaji kodi, rushwa, ufisadi, ubinafsi na kutokuwa na uzalendo.

“Katika tafiti hii tumegundua kuwa Lowassa anaongoza katika kila nyanja kama Rais pendekezwa kuwa Rais wa Tanzania 2015, ukiangalia jinsia zote wa kiume na wa kike wanamtaka Lowassa kuwa Rais,” alifafanua na kuongeza:

“Tafiti hii inaipa chama dira na mwelekeo wa kujua kwamba ni Mtanzania gani ndani ya chama anayehitajika na Watanzania, chama kikishajua hilo hakifanyi kosa kumwacha mtu huyo anayehitajika na Watanzania ili kwanza kukiokoa chama kupoteza dola lakini pia kukilinda kiweze kubaki madarakani.”

Aliasema chama mbadala wa CCM ni Chadema, takwimu zinaonyesha kuwa, iwapo Lowassa hatapeperusha bendera ya CCM 2015, basi anayetakwa na wananchi kuwa Rais mbadala ni Dk. Willibrod Slaa.

Alisema Machi 2015, taasisi isiyo ya kiserikali ya Positive Thinkers Tanzania ripoti yake ya utafiti  ilioji watu 3,298 na Lowassa alipata watu 752 katika mikoa 13 Tanzania Bara na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,Tibatizibwa Yabutinga, alielezea kuwa Lowassa ni mwanasiasa anayekubalika sana kuwa rais ajaye 2015.

 Alisema katika ripoti hiyo ili orodhesha matokeo yake kuwa Lowassa alipata asilimia 22.8, Slaa  19.5 asilimia ,  Nchemba 10.6, Profesa Lipumba 8.9, John Magufuli 6.8 , Kabwe 6.7, Membe 5.9, Pinda 3.2 ,  makamba 1.6,  Mwandosya 1.2.

Alisema Twaweza sauti za Wananchi, Nov.2014 Imegundua kuwa katika watu 1,445 walioshiriki utafiti ni kuwa wengi wao walisema kuwa changamoto kuu ni Uchumi, elimu na afya na wanasiasa wengi hawatimizi ahadi zao.

Twaweza pia wametoa tafiti kuwa CCM bado kinapendwa na Watanzania kwa asilimia 51 kwa nafasi ya urais, asilimia 46 kwa nafasi ya ubunge na kwa asilimia 47 kwa nafasi za udiwani ikifuatiwa na Chadema.

Alisema ripoti hiyo  ya Twaweza pia inatoa ripoti kuwa vijana chini ya miaka 34, watu chini ya miaka 50 na wazee zaidi ya miaka 50 kwa pamoja wengi wana sapoti kubwa kwa chama cha mapinduzi, na katika nafasi ya urais 2015, ripoti ya Twaweza inasema kuwa ndani ya CCM, kura za wagombea urais kwa tiketi ya CCM ni  Lowassa anaongoza kwa asilimia 17, Pinda asilimia 14, Magufuli asilimia tano, Samuel Sitta asilimia tano, Membe asilimia saba.

Alisema ripoti hiyo ya Twaweza pia iliweka wazi kuwa iwapo uchaguzi utafanywa , basi CCM itaongoza kwa asilimia 47, Ukawa kwa asilimia 28 na kama mtu atasimama binafsi, basi atapata asilimia 19.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa