Jumatano, 6 Mei 2015

MTOTO ATOA USHUHUDA WA POLISI KUHUSU UNYAMA ALIOFANYIWA BABA YAKE BAADA YA POLISI KUMGONGA!!

Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support ya jijini Dar, Octavian Nandi Mpendakazi.
Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support ya jijini Dar, Octavian Nandi Mpendakazi (60), hali yake ni mbaya kwa kile kinachodaiwa aligongwa na gari la polisi na kuvunjika mbavu, mguu wa kushoto mara mbili pia kakatika utumbo siku ya Sikukuu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.Mtoto wa majeruhi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Rose Nandi, akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, alidai kwamba baba yake aligongwa na gari la polisi wakati akivuka barabara Aprili 26, mwaka huu eneo la Tazara, Dar.
“Nilipoenda eneo la tukio niliambiwa na walioshuhudia kwamba baba aligongwa na ‘defender’ la polisi,” alisema mtoto huyo.Aliendelea kusema kwamba, baba yake aligongwa saa kumi na mbili na nusu asubuhi na gari hilo lililokuwa likitokea Gongo la Mboto kwenda Uwanja wa Taifa kwenye sherehe za Muungano.
“Siamini kama baba atapona na hata kama atapona lakini tayari wameshamtia ulemavu, siku ya tukio nilipigiwa simu na mdogo wangu akanifahamisha baba aligongwa na gari la polisi na hali yake ilikuwa mbaya sana.
Octavian Nandi Mpendakazi akiwa hoi hospitalini.
ALIKUWA ICU
“Nilipopata taarifa hiyo nilikwenda Hospitali ya Temeke nilikoelezwa alipelekwa lakini sikumuona, nilihisi huenda amefariki, nilipowauliza wauguzi waliniambia alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).“Tulikaa pale kwa muda mrefu, baadaye akarudishwa wodini, nilimsemesha wala hakuongea nikajua amepoteza fahamu.
“Alikuwa akitokwa machozi kitendo kilichonifanya nibubujikwe na machozi, nilishindwa kujizuia kwani baba alibadilika sana, alipochunguzwa ilibainika amevunjika mguu wa kushoto mara mbili, mbavu, utumbo ulikatika na sehemu nyingine ilikuwa na matobo.
POLISI WATAJWA
“Baadaye nilifuatana na ndugu zangu hadi eneo la tukio, wananchi waliokuwa pale walisema aligongwa na gari la polisi ambalo namba zake hawakuzishika na likamsukumiza katika mtaro na hawakumpa msaada ndipo wananchi walipojitokeza kumsaidia na kumpeleka hospitalini.
“Nilijisikia vibaya sana nilipoambiwa hivyo na kujiuliza kwa nini polisi wafanye hivyo? Ajali sawa, lakini si wangempa msaada mtu waliyemgonga? Mpaka ninapoongea na wewe hawajafika kumjulia hali baba hapa hospitalini, huu ni unyama.“Nitahakikisha nawafungulia kesi polisi hao kwani wanajua ni gari gani lilikuwa maeneo hayo muda huo.
Jeraha alilolipata mguuni.
AFANYIWA UPASUAJI
“Kwa sasa amefanyiwa upasuaji tumboni, kifuani na mguuni mara mbili, kuna dawa ambazo hazipo hapa hospitalini, natakiwa nizinunue, kwa kweli nimechanganyikiwa kwa kuwa sina fedha za matibabu na polisi wametutelekeza,” alisema Rose.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Andrew Masatya Satta alipoulizwa na mwandishi wetu kama ana taarifa juu ya tukio hilo alisema halijamfikia. “Sijapata taarifa hiyo lakini nitafuatilia,” alisema kamanda huyo.
Kwa yeyote aliyeguswa na tukio hili na anapenda kumsaidia Rose katika tatizo linalomkabili mzazi wake, awasiliane naye kwa namba 0719 175717.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa