Jumatatu, 4 Mei 2015

Mitihani Kidato cha sita Yaanza

Wanafunzi wa Kidato cha Sita wa  Shule ya Sekondari ya Coaster High School wakijisomea jana kabla ya kuingia katika chumba cha mtihani  ambapo mtihani wa kitaifa ulianza jana nchi nzima.

MTIHANI wa kidato cha Sita uliyoanza jana kote umeendelea licha ya mgomo wa madereva uliofanyika nchini nzima na kusababisha tatizo la usafiri.
 
MPEKUZI ilifanikiwa kuzunguka katika baadhi ya shule zilizopo katikati ya jiji la Dar es Salaam ambazo ni Tambaza, Jangwani na Azania na kukuta wanafunzi wanaendeleea na mitihani yao.
 
Hata hivyo baadhi ya walimu waliuambia mtandao huu kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wamechelewa kufika katika chumba cha mtihani kutokana na tatizo la usafiri.
 
“Wakati nikiwa katika kituo cha daladala eneo la Ubungo niliona wanafunzi wawili wa shuleni kwetu wakitembea kwa miguu ili wakafanye mtihani, ilibidi niwakodishie bajaji ili wawahi mitihani yao,” alisema mwalimu huyo anayefundisha katika Shule ya Azania.
 
Akizungumza na MPEKUZI Waziri  wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa, alisema mgomo wa vyombo vya usafiri unaoendelea haujaathiri kwa namna yoyote mitihani hiyo.
 
Alisema alifanikiwa kutembelea baadhi ya shule na hakuna taarifa zozote za mwanafunzi kushindwa kufanya mitihani kutokana na mgomo huo.
 
 “Huu mgomo ulioanza leo (jana) hauna uhusiano wowote na mitihani iliyoanza kwa sababu asilimia kubwa ya wanafunzi hawa wanakaa kwenye mabweni” alisema Dk Kawambwa.
 
Alisema hata hivyo wale  wanaoishi nyumbani wameweza kufanikiwa kufika kwenye vituo vyao vya kufanyia  mitihani na kuwasifu wazazi kwa kuhakikisha wanawahi.
 
“Nawasifu wazazi na walezi wote kuwawezesha wanafunzi kufika kwa wakati  pamoja na changamoto hiyo, ingawa sijui wametumia njia gani” alisema Dk Kawambwa.
 
Alisema amewasiliana na maofisa wasimamizi wa elimu nchi nzima juu ya hali halisi na taarifa alizonazo ni kuwa vituo vyote vimefunguliwa kwa wakati unaotakiwa bila ya matatizo.
 
Mtihani wa kidato cha Sita umeanza Mei 4 na unatarajiwa kumalizika Mei 27, mwaka huu ambapo jumla ya watahiniwa 40,758 kati ya hao wa Shule ni 35,585 na wakujitegemea ni 5,373.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa