Ijumaa, 10 Aprili 2015

Huyu Ndo Mtanzania Anayetuhumiwa Kwa Ugaidi Kenya.....Jana Alifikishwa Mahakamani Chini Ya Ulinzi Mkali


Mtanzania anayedaiwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa – Kenya, Rashid Charles Mberesero, jana alifikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja wakati polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.
 
Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.
 
Mahakama jijini Nairobi ilisema jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma hizo na wenzake wanne watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.
 
Haikufahamika mara moja sababu za kuamuliwa kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa kueleza kuwa ‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.
 
Mwendesha Mashtaka, Daniel Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa Mtanzania huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, alikuwa amepanga safari ya kuelekea Somalia kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi.
 
Watuhumiwa hao ni kati ya 14 waliotiwa mbaroni hivi karibuni baada ya shambulizi hilo la kigaidi.
 
Mahakama hiyo pia imewaamuru washukiwa wengine kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda wa siku tano hadi 15.
 
Awali, Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa polisi walikuwa wakifuatilia kwa karibu uhusiano baina ya wale waliofanya shambulizi hilo na mfanyabiashara mmoja anayemiliki hoteli mjini Garissa. Inasemekana kuwa watu waliotekeleza shambulio hilo walikuwa wamelala katika hoteli hiyo.
 
Hakula chakula cha shule
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kigwe, mkoani Dodoma alipokuwa akisema Mberesero baada ya kufaulu kutoka Gonja, wamesema hakuwahi kula chakula chochote shuleni kwa kipindi cha mwezi mmoja aliokaa akisubiri kuhamishwa na kubadilishiwa mchepuo wa masomo.
 
Wakizungumza na mwandishi wetu shuleni hapo jana, wanafunzi wa kidato cha tano, Yoram James na Thomas Godwin, walisema siku zote alizoishi shuleni hapo alikuwa akila kwa mama lishe jirani na shule hiyo.
 
“Lakini alikuwa na mkarimu kwetu wakati mwingine alikuwa akitununulia maandazi ya kunywea chai,” alisema Yoram.
 
Hata hivyo, walisema kutokana na upole wake, jinsi anavyoongea na kutumia muda mrefu msikitini, walimpa jina la Ustaadhi.
 
“Alikuwa akienda mjini mara kwa mara, nadhani alikuwa akiomba ruhusa kwa walimu au alikuwa akitoroka,” alisema Thomas.
 
Thomas alisema Rashid alikuwa akipenda kucheza mpira wa miguu kwa hiyo alitenga muda wake kwa ajili hiyo.
 
Uhamisho wake
Mkuu wa Shule hiyo, Ramadhan Bakari alisema ofisi ya elimu mkoa ilituma taarifa ya kuwataka wanafunzi wanaopenda kubadilisha mchepuo kuandika barua ya maombi.
 
“Rashid alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi watano walioomba kubadilishiwa mchepuo kutoka Sanaa kwenda Sayansi, walikubaliwa wanne akiwamo yeye,” alisema Bakari.
 
Hata hivyo, mwalimu huyo alisema Rashid alikuwa akihangaika ahamishiwe Shule ya Sekondari ya Bihawana, tangu aliporipoti Kigwe.
 
“Hatuwezi kuzungumza kuhusu tabia zake maana hapa hakuishi siku nyingi, alikuwa kama yuko njiani,” alisema.
 
“Aliondoka hapa shuleni kwenda Bihawana Agosti 19, mwaka jana baada ya taratibu kukamilika,” alisema.
 
Uvumi wasambazwa
Hofu imetanda katika maeneo mbalimbali baada ya kusambazwa ujumbe kwenye simu na mitandao ya kijamii ukidaiwa kutolewa na Umoja wa Mataifa (UN) kutahadharisha watumishi wake waepuke kukaa katika makundi makubwa na mikusanyiko katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha leo kuepuka mashambulizi ya kigaidi.
 
Hata hivyo, Msemaji wa UN, Usiah Ledama alikanusha umoja huo kuhusika na ujumbe huo akisema ni feki na hauna ukweli wowote.
 
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Diwani Athumani alisema hata kama ujumbe huo ni feki, bado Jeshi la Polisi linachukua tahadhari kuhakikisha Taifa linakuwa salama.
 
“Huo ujumbe uwe feki au wa kweli, lazima tuchukue tahadhari, Tanzania si kisiwa, tutakuwa salama kwa asilimia 100, kwa hiyo ulinzi unaimarishwa,” alisema.
 
Alisema ni lazima kila mtu awe mlinzi wa mwenzake na ahakikishe kuwa anakuwa mzalendo kwa kutoa taarifa zozote ambazo anadhani zitalisaidia Jeshi la Polisi katika ulinzi.
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa