MAMLAKA nchini Burundi zimekata mawasiliano ya mitandao ya kijamii kupitia simu za mkononi, ambayo yamekuwa yakitumika kupanga maandamano ya kumpinga Rais Pierre Nkurunziza.
Mamia ya waandamanaji wako barabarani kwenye mji mkuu wa Burundi,
Bujumbura kwa siku ya nne jana wakipinga uamuzi wa Nkurunziza kuwania
urais kwa muhula wa tatu.
Mawasiliano hayo ni kupitia mitandao ikiwamo ya Facebook, Whatsapp,
Twitter na Tango huku kituo kikuu binafsi cha redio kikiwa kimefungwa
katika harakati za Serikali kuzuia kuenea kwa ujumbe unaohamasisha
maandamano.
Mitandao ya jamii imekuwa ikitumika kuratibu maandamano hayo ambayo ni
makubwa zaidi nchini Burundi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa
wenyewe mwaka 2005.
African Public Rasio, maarufu kama ‘Sauti ya Wasio na Sauti’, ni moja ya
vituo vitatu vya redio ambavyo matangazo yake ya moja kwa moja
yamesitishwa, kwa kile Serikali ilichodai kuwa vinavuruga amani.
Nkurunziza, kiongozi wa zamani wa waasi ameonya kuwa yeyote anayetaka
kusababisha matatizo kwa chama tawala atajiweka mwenyewe matatani.
Watu watatu wameuawa tangu Jumapili wakati polisi walipoutawanya umati
kwa risasi za moto huku makumi kwa maelfu wakiikimbia nchi.
Chini ya Katiba ya Burundi, marais wanaweza kuchaguliwa kwa mihula
miwili , lakini washirika wa Nkurunziza wanasema muhula wake wa kwanza
hauhesabiki kwa vile aliteuliwa na Bunge.
Nkurunziza yu madarakani tangu mwaka 2005, wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 12 vilipomalizika rasmi.
Watu zaidi ya 300,000 waliuawa katika mgogoro huo baina ya jeshi
lililodhibitiwa na Watutsi walio wachache na makundi ya waasi wa Kihutu
kama vile CNDD-FDD la Nkurunziza.
Mpekuzi blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni