WAZIRI
wa Habari, Vijana Utamuduni na Michezo, Dk. Fennela Mukangara
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kukabidhi Kombe la
Ubingwa wa Ligi Kuu Bara klabu ya Yanga, Mei 6 mwaka huu katika mchezo
kati ya Azam FC dhidi ya timu hiyo.
Yanga
imetwaa ubingwa huo Jumatatu hii ikiwa ni mara ya 25 tangu ilipoanza
kushiriki ligi hiyo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya
timu ya Polisi Morogoro katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa,
huku ikiwa bado na michezo miwili mikononi kabla ya ligi hiyo
kumalizika.
Baada
ya mechi hiyo Yanga ilifikisha jumla ya pointi 55 ambazo haziwezi
kufikiwa na timu nyingine hata Azam ambao wapo nafasi ya pili wakiwa na
pointi 45 na michezo miwili mkononi.
Yanga imewavua rasmi ubingwa huo Azam ambao ndio walikuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo ambalo walitwaa msimu uliopita.
Katika
hatua nyingine Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
ametuma salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji
kufuatia timu yake kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu hiyo msimu wa 2014/2015.
Katika
salamu zake, Malinzi amesema kutwaa Ubingwa wa VPL ni jambo muhimu na
sasa wanapaswa kuanza maaandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa
barani Afrika mwakani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni