Jumatano, 8 Aprili 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akutana na Balozi Mdogo Mpya wa India Zanzibar


Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akipokea zawadi kutoka kwa Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  ameyashauri  Makampuni  na Taasisi za uwekezaji  kutoka Nchini India kuwekeza miradi yao katika Visiwa vya Unguja na Pemba  ili kuitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukaribisha wawekezaji  mbali mbali kuwekeza hapa Nchini.
Alisema India  bado ina nafasi pana  kwa Makampuni yake kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi hasa katika Sekta ya Viwanda kama ilivyowahi kutumia fursa hiyo hapa Zanzibar katika miaka ya 80.
Akizungumza na Balozi Mdogo  Mpya wa India hapa Zanzibar  Bwana  Satendar Kumar hapo Ofisini kwake Vuga  Mjini Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Sekta ya Viwanda  ni eneo muhimu katika kukuza uchumi na kupunguza Umaskini.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa na malengo la kuimarisha sekta hiyo kwa azma ya  kulisaidia kundi kubwa la Vijana wasio na ajira ambalo limekuwa likiongezeka kila mwaka baada ya kumaliza masomo yao.
Akizungumzia miradi mengine ya Kiuchumi na Maendeleo ya Kijamii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliiomba Serikali ya India kupitia Balozi wake Mdogo  huyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati za Maendeleo kwenye sekta hizo.
Mapema Balozi Mdogo Mpya wa India hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba uhusiano wa Kidiplomasia kati ya India na Tanzania ikiwemo Zanzibar utaendelea kuimarishwa siku hadi siku.
Balozi Satendar alisema uhusiano huo umejengwa katika mpango Maalum wa Maendeleo wa India – Afrika  uliojikita kwa Wataalamu wa Nchi hiyo kusaidia taaluma katika sekta za afya, elimu, miradi ya Kazi za amali pamoja na Teknolojia ya Mawasiliano na Habari.
Michuzi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa