Alhamisi, 30 Aprili 2015

IRAQ: Wapiganaji 91 wa Kundi la Dola la Kiislamu (IS) Wauawa


WAPIGANAJI 91 wa kundi la Dola la Kiislamu (IS) wameuawa na jeshi la Iraq lililokuwa likisaidiana na wapiganaji wa kujitolea katika sehemu mbalimbali huko nchini Iraq.

Wapiganaji hao waliuawa katika matukio mawili tofauti wakati vikosi vya jeshi la Iraq vilipokuwa vikipambana na wapiganaji hao.

Vyombo vya habari nchini Iraq vimetangaza kuwa Wizara ya Ulinzi ya Iraq imetoa taarifa kuwa vikosi vya Iraq vimewaua wapiganaji 61 wa kundi la IS  na kuteketeza maficho manne ya wapiganaji hao.

Taarifa hiyo imesema kuwa magari manne ya kijeshi ya wapiganaji wa kundi la IS yajulikanayo kama Humvee ambayo yalikuwa yamesheheni silaha za milipuko pamoja na malori sita yaliyokuwa na silaha yameteketezwa.

Jeshi la Iraq na vikosi vya kujitolea vilifanya operesheni hiyo dhidi ya kundi hilo katika mji wa al Karmah umbali wa kilomita 16, kaskazini mashariki mwa Fallujah.

Mkoa wa Fallujah ni miongoni mwa mikoa ambayo imekumbwa na machafuko wa al-Anbar.

Katika tukio jingine tafauti vikosi vya Iraq vimewaua magaidi 30 wa kundi hilo na kutegua bomu moja lililokuwa limetegwa katika lori wakati vikosi vya Iraq vilipokuwa vikipambana na magaidi hao katika mji wa Ramadi.

Mji wa Ramad upo umbali wa kilomita 110 magharibi mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa