Serikali imerejesha mafunzo ya madereva kila baada ya miaka mitatu wakati wa kumalizika kwa muda wa leseni zao, huku ikifafanua kuwa elimu watakayoipata ina umuhimu katika kazi zao, kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika sekta hiyo.
Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, alitangaza uamuzi huo wa
Serikali jana katika mkutano kati yake na viongozi wa madereva wa mabasi
nchini.
Mkutano
huo umefanyika kama ilivyoahidiwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka, wakati alipokuwa akijitahidi kumaliza mgomo wa madereva
uliofanyika Aprili 10 mwaka huu, wakati walipokuwa wakipinga pamoja na
mambo mengine, sharti la kwenda shule ili kupata leseni mpya.
Madereva
hao walitaka Serikali ifanyie marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani,
kwa kuondoa kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya muda mfupi kila wakati leseni zao
zinapoisha, ili kupata sifa ya kupata leseni nyingine.
Sababu
ya kupinga kupata mafunzo, ilidaiwa kuwa utaratibu huo uliotangazwa
Machi 30, mwaka huu, ulianzishwa bila kushirikisha madereva katika
kuuandaa.
Pia
walipinga kutakiwa kujilipia gharama za shule hiyo ambazo walidai ni Sh
560,000 kwa magari ya kawaida na Sh 200,000 kwa magari ya abiria.
Sababu
nyingine iliyochangia wapinge shule hiyo, walidai ni kukosekana kwa
mikataba ya ajira, inayoweza kuwahakikishia kulindwa kwa kazi zao hadi
wanapomaliza mafunzo.
Madai
mengine yaliyokuwa nje ya shule hiyo, madereva hao walitaka kuondolewa
kwa faini ya Sh 300,000 kwa kila kosa la barabarani na kuitaka Mamlaka
ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), kuhakiki
uhalisia wa dereva anayeandikishwa na mmiliki wa chombo husika.
Majibu
ya Serikali Mahanga aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alisoma tamko
la Serikali lililoeleza kuwa pamoja na kurejesha mafunzo hayo,
utekelezaji wake hautafanyika mara moja kwa kuwa Kanuni zake
hazijakamilika.
“Tangazo
hili (la kwenda shule) limetolewa kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo
kazini kwa wafanyakazi na madereva kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine,”
alisema Mahanga.
Alisisitiza
kuwa baada ya miaka mitatu ya leseni, dereva atatakiwa kupata mafunzo
mafupi, ambayo ni kati ya siku tatu hadi saba na atakayegharimia mafunzo
hayo ni mwajiri, si mfanyakazi na ni katika chuo chochote
kinachotambulika.
Akifafanua,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwamini Malemi aliyekuwepo
katika mkutano huo, alisema mitaala ya mafunzo hayo bado inaandaliwa,
hivyo si rahisi Kanuni hiyo kuanza kutekelezwa mwaka huu hata kama
zitakamilika.
Kuhusu
mikataba ya ajira ambayo ililalamikiwa mno na madereva wakati wa mgomo,
Mahanga alisema Serikali itapitia upya mikataba hiyo ili kuhakikisha
mambo yote muhimu yanazingatiwa.
Akiongezea
hoja katika suala la mikataba, Malemi alisema ni lazima mikataba iwe
imekamilika kabla ya kuanza kutumika kwa kanuni ya kwenda shule, ili
ioneshe wajibu wa mwajiri katika kumsomesha mfanyakazi.
Kuhusu
kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova ya kuondoa tochi za kupima mwendo kasi barabarani, Mahanga
alisema matumizi ya tochi zinazotumika kupima mwendo kasi na ratiba ni
sehemu ya utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani.
Hoja
nyingine Katika kikao hicho mbali na hoja zilizosababisha mgomo,
kulikuwa na hoja nyingine zilizowasilishwa, ikiwemo changamoto ya
madereva kupata maelekezo yanayokinzana kutoka Jeshi la Polisi na
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), kuhusu
ratiba ya kuondoka wanakotoka na kuwasili wanakokwenda.
Akitoa
majibu ya Serikali, Mahanga alisema amepokea hoja hiyo na ataifanya
utafiti wa kina. Katika hoja ya kuwataka waajiri kuongeza posho za kazi,
Mahanga alisema Serikali haiwezi kupanga posho za madereva katika kikao
hicho, kwasababu kila mwajiri ana uwezo wake kulingana na safari za
gari yake.
Hata
hivyo, aliahidi kufanyika utafiti suala hilo katika nchi nyingine, ili
aone namna ambavyo madereva wengine wamekuwa wakilipwa posho.
Serikali
pia imeahidi kuimarisha ukaguzi sehemu za kazi kwa kushirikiana na
Sumatra, utakaohusu wamiliki wa magari na kuhuisha mfumo wa kumbukumbu,
utakaoonesha kila gari na dereva wake halisi na kuweka vitambulisho vya
dereva katika kila gari analoendesha.
Mahanga
alisema Serikali pia itaweka utaratibu mpya ambapo dereva mwenyewe
atajiwekea bima ya ajali itakayoanzishwa na kujiunga na vyama vya
wafanyakazi, ili watetee mikataba yao ili iweke pia maswala ya bima
hizo.
Alisema pia Serikali imeanzisha Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi, ambao utaanza hivi karibuni, ambao mwajiri atawajibika kuchangia.
Chama cha Wafanyakazi
Kuhusu
chama cha wafanyakazi, Mahanga alisema Serikali imepokea pendekezo la
kusaidia madereva kuunda chama cha wafanyakazi chenye nguvu, ambapo
alisema kumbukumbu zinaonesha madereva wana vyama vilivyosajiliwa kwa
Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.
Alitaja
vyama hivyo kuwa ni Umoja wa Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafiri
Tanzania (COTWU), kilichosajiliwa mwaka 2000 na Chama cha Wafanyakazi
cha Usafiri wa Barabara (TARWORTU) kilichosajiliwa mwaka 2013.
“Katika
kushughulikia changamoto za wafanyakazi na mwajiri wote mnategemeana,
jambo mtakalofanya ni kuanzisha majadiliano kupitia vyama vya
wafanyakazi lakini kwanza muwe ndani ya vyama,” alisema Mahanga.
Wanung’unika
Baada
ya kusomwa kwa tamko hilo la Serikali, Katibu Mkuu wa Vyama vya
Madereva Tanzania, Mwanarashidi Salehe, alisema mafunzo wanayotakiwa
kuchukua hayana tija yoyote, kwa kuwa wakufunzi ni wa kizamani na pia
magari yanayotumika ni ya kizamani, ambayo hayaongezi chochote katika
kazi yao.
“Kwanza
hakuna kipya katika mafunzo hayo, mimi nimehudhuria mara mbili....pili
katika kikao hiki tulitarajia tutakutana na wamiliki wa magari ambao
ndio waajiri wetu ili waseme waliyonayo juu yetu na sisi tuseme yetu
tujadiliane na kupata majibu,” alisema Salehe.
Mwenyekiti
wa chama hicho, Clement Masanja alisema mikataba waliyonayo madereva ni
dhaifu mno, haioneshi mambo ambayo dereva atanufaika nayo.
“Tulitarajia
katika kikao hiki tutatoka na majibu ya posho za madereva, ili dereva
ajue atalipwa kiasi gani kwa safari za ndani na nje ya nchi kwa sababu
anavyolipwa ni manyanyaso matupu,” alisema Masanja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni