BAADA
ya watani zao wa jadi Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu vita ya kuwania
kushiriki michuano ya kimataifa sasa mwakani imesalia kwa vigogo wengine
wa soka nchini Simba SC na Azam FC.
Yanga
SC kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu imekata tiketi ya kushiriki michuano
ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, huku wakiziachia kivumbi Simba na
Azam ambazo mechi zao za mwisho katika Ligi Kuu ndizo zitaamua nani
atatwaa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kwa
namna hali ya mambo ilivyo, Simba ili kupata tiketi hiyo inalazimika
kukesha usiku na mchana kuomba dua wapinzani wao Azam wapoteze mechi zao
za mwisho ili kupata tiketi hiyo ambayo wanaisotea kwa miaka mitatu
bila mafanikio.
Simba
ipo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 41 nyuma ya Azam waliopo nafasi ya
pili wakiwa na pointi 45, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi wanapanga
kuwafanyia kitu mbaya Wanalambalamba hao katika mchezo utakaozikutanisha
timu hizo Jumamosi wiki hii.
Iwapo
Azam itashinda dhidi ya Simba ni wazi wekundu hao wa Msimbazi
wamepoteza tiketi ya CAF kwa msimu wa nne, kwani hawataweza kuzifikia
pointi za Wanalambalamba.
Itakumbukwa Azam licha ya kuizidi Simba kwa pointi nne pia ina faida ya mchezo mmoja mkononi.
Kama
Simba watashinda mchezo huo itabidi waungane na mashabiki wa Yanga
kuwashangilia mabingwa hao wapya watakapocheza na Azam FC, ili kuzidi
kutanua wigo wa kufukuzia nafasi ya pili hali inayofanya vita ya kuwania
tiketi ya CAF kuwa na uhondo wa aina yake.
Simba
wamebakiwa na michezo miwili dhidi ya Azam FC na JKT Ruvu, huku Azam
wakibakiwa na michezo mitatu dhidi ya Yanga na Mgambo JKT Ruvu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni