Siku moja tu baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, kutangaza usalama wa maisha yake kuwa hatarini, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameibuka na kudai tuhuma alizohusishwa dhidi ya Mengi si za kweli.
Dk.
Mengi, alitangaza hofu yake juzi, wakati alipokutana na vyombo
mbalimbali vya habari, kufuatia gazeti moja linalochapishwa kila wiki
kuandika kuwa Rais Jakaya Kikwete, ameahidi kupambana na Mengi baada ya
kuelezwa kuwa anaihujumu serikali yake.
Zitto
alihusishwa katika habari hiyo kuwa ndiye anayedaiwa kwenda kwa Rais
Kikwete kumweleza kuwa Mengi anaihujumu serikali yake baada ya kutolewa
kwa ripoti ya PAC.
Alisema
taarifa maalum ya Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu
ufisadi wa Sh. Bilioni 306 za Escrow, haihusiani kwa namna yoyote na Dk.
Mengi.
Zitto
alisema kuwa watu wanaomhusisha mfanyabiashara huyo na mkakati wa
kuihujumu serikali ya Rais Kikwete ni wale waliokosa hoja baada ya
masuala yao ya kuwahujumu Watanzania kukwama kufuatia ripoti ya PAC
kuwaumbua.
Zitto alitoa kauli hiyo jana katika uwanja wa mahakama ya Mwanzo mjini Shinyanga.
Katika
hofu yake, Dk. Mengi alisema ameshangazwa na ukimya wa Ikulu na Idara
ya Habari Maelezo, pamoja na habari hiyo kuchapishwa kwenye gazeti
ikimhusisha Rais.
"Mengi
sio mbunge, sio mjumbe wa PAC na hakushawishi PAC kwa namna yeyote ile.
Wezi wa Escrow wasitapetape kutafuta mchawi wakati mchawi ni wizi wao
wenyewe," alisema Zitto.
"Habari
zilizoandikwa kwenye gazeti la Taifa Imara zinazomhusu Regnald Mengi
na Rais Jakaya Kikwete si za kweli, ni fitina zimetengenezwa," alisema.
Zitto,
aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC, alisema habari iliyoandikwa na gazeti la
Taifa Imara la Machi 23, mwaka huu, zinazoonyesha kuwa alikutana na Rais
kwa msaada wa watu mbalimbali, ni mwendelezo mwingine wa porojo za watu
walioathiriwa na uamuzi wa PAC katika sakata la Escrow.
"Habari
hiyo ilibeba maudhui ya 'post' iliyoandikwa katika mtandao wa
Mwanahalisi online, inaonyesha kuwa mimi nilikutana na Rais kwa msaada
wa watu mbalimbali na katika kikao hicho inadaiwa nilisema kuwa Mengi
ndiye aliyechochea wabunge kuishughulikia serikali ya Rais Kikwete ili
ianguke,” alisema.
Zitto
alisema hahitaji kutumia watu kwa ajili ya kukutana na Rais Kikwete,
kwa kuwa suala hilo linawezekana kufanyika katika taratibu za kawaida za
kiserikali.
Alisema
kitendo cha gazeti hilo kudai kuwa aliomba watu wamkutanishe na Rais,
inaonyesha namna mwandishi alivyoshindwa kutunga uongo wake.
“Hadithi ya kwamba nimeomba watu wanikutanishe na Rais inaonyesha namna mwandishi alivyoshindwa kutunga uongo wake.
Katika
kukutana kwangu na Rais kikazi sijawahi hata mara moja kuzungumzia
watu. Hivyo kusema nilikwenda Ikulu kumzungumzia Mengi ni kunidharau na
kuidhalilisha Taarifa ya Urais,” alisema.
Alisema
ifahamike kuwa gazeti la Taifa Imara linamilikiwa na James Rugemalira
wa kashfa ya Escrow na kuendeshwa na Prince Bagenda, aliyeandaa mkutano
wa mmoja wa mawaziri waliofukuzwa kazi kwa kashfa hiyo.
Aliongeza
kuwa hata chanzo cha habari hiyo ni mtandao wa Mwanahalisi online ambao
unaoendeshwa na mmiliki wa Mawio, gazeti ambalo kila wiki lina habari
za kutunga dhidi yake na chama chake.
Aidha,
alisema kama kuna mtu ana chembe ya ushahidi wa jambo hilo apeleke
kwenye vyombo vya dola kwa hatua kuliko kurudia rudia porojo hizo kwenye
vyombo vya habari.
Alisema
kwa sababu hiyo amemwelekeza mwanasheria wake achukue hatua za kisheria
dhidi ya gazeti la Taifa Imara na gazeti la Mawio, kwa mfululizo wa
habari za kutunga uongo dhidi yake kila kukicha.
Juzi
Mengi alitoa taarifa katika vyombo vya habari akielezea hofu yake juu
ya ukimya wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, pamoja na Idara ya habari
maelezo kufuatia taarifa iliyoandikwa na gazeti la Taifa Imara la Machi
23 mwaka huu.
Mwandishi
alizungumza kwa njia ya simu na Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Assah
Mwambene, na kujibu kwa mkato "no comment my dear" (sina cha
kuzungumza).
Mpekuzi blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni