Jumatano, 29 Aprili 2015

Rais Kikwete Azindua Meli Mbili Za KIVITA Kwa Kishindo Jijini Dar


RAIS Jakaya Kikwete, jana amezindua na kuzitunukia Kamisheni meli mbili za kivita za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Kamandi ya Wanamaji ambazo zitatumika kufanya doria na kulinda mipaka ya majini katika Bahari ya Hindi.

Meli hizo zimepewa majina ya P77 Mwitongo na P78 Msoga zenye urefu wa mita 60 na zina uwezo wa kufanya doria katika kina kirefu cha maji.

Rais Kikwete alisema, kupatikana kwa meli hizo kumeifanya Tanzania kuandika ukurasa mpya wa uhusiano kati yake na China ambao uliasisiwa na waasisi wa mataifa hayo hayati Mwalimu Nyerere na Mao Tse Tung.

Alisema meli hizo zimekuja nchini kwa msaada wa Serikali ya Watu wa China zikiwa na uwezo wa kubeba silaha nzito kila moja ikiwa na mizinga miwili mikubwa na midogo sita.

"Jeshi letu la Wanamaji wakati linaanzishwa 1971, lilisaidiwa na Serikali ya China meli 13, rada na wataalamu wetu kupatiwa nafasi mbalimbali za mafunzo...meli hizi zitatuongezea ulinzi katika mipaka yetu majini.

"Kilio kikubwa cha jeshi letu kilikuwa uwezo mdogo wa meli zetu, tumekuwa na kazi ya kutafuta meli hizo na sasa tuna mpango wa kuchukua meli nyingine kubwa zaidi zenye uwezo, kilichobaki ni taratibu za kifedha tu," alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, lazima Tanzania ijenge uwezo wa kulinda mali zetu, mipaka, samaki na mitambo ya gesi ambayo imesimikwa baharini hivi karibuni.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi, Dkt. Hussen Mwinyi, alisema Serikali ya China imekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema jeshi hilo limepiga hatua katika ununuzi wa dhana za kivita na kuendeleza mafunzo ya kijeshi.
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mara baada ya kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam jana April 28, 2015
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata picha ya kumbukumbu na makamanda wa meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam jana April 28, 2015
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Chifu Edward Wanzagi wa kabila la Wazanaki (kati) pamoja na Mbunge wa Afrika Mashariki Mhe Makongoro Nyerere baada ya kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam jana April 28, 2015.
 
(PICHA NA IKULU)
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa