Alhamisi, 30 Aprili 2015

Kaseja, Mgosi Wagoma Kurudi Simba


WAKATI kukiwa na tetesi za Simba kutaka kuwarudisha kundini wachezaji wake wa zamani Juma Kaseja na Mussa Hassan ‘Mgosi’ ili kuimarisha kikosi chao msimu ujao, wachezaji hao kila mmoja ametoa lake la moyoni.
 
Wakizungumza na MPEKUZI  kwa nyakati tofauti walisema hawajafanya mazungumzo yoyote na Kamati ya Usajili ya Simba ingawa taarifa za wao kutakiwa wanazisikia tu mitaani.

Musa Mgosi alisema yeye ana mkataba na timu yake ya Mtibwa Sugar na kwamba hana mpango wowote wa kwenda timu nyingine na badala yake anataka kumalizia soka lake Manungu.

 “Nimeshawahi kucheza Simba naiheshimu kama timu iliyonifanya nijulikane lakini sasa huu ni muda wa wengine kuipa mafanikio, kwani upande wangu nafikiria kumalizia soka langu Mtibwa,” alisema Mgosi.

Kipa Juma Kaseja alisema hana taarifa juu ya suala hilo na kama lipo atapewa taarifa na meneja wake ambaye anamsimamia kwa kila kitu katika soka.

 “Sijui chochote kuhusu kutakiwa na timu yoyote ile, ninachotambua niko huru nafanya mazoezi binafsi, pia masuala yote yanayonihusu yako chini ya meneja wangu muulizeni yeye,” alisema.

Mbali ya wachezaji hao, pia straika wa Coastal Union, Rama Salim naye amehusishwa na kutakiwa na Wekundu hao wa msimbazi ambapo alisema bado ana mkataba na klabu yake hiyo na kama kutatokea mengine itategemea na makubaliano ya pande zote mbili.

Kwa upande wake mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Ame Ally alisema bado ana mkataba na timu yake hiyo lakini lolote linaweza kutokea kwenye soka kama makubaliano ya pande zote yataafikiwa.
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa