Jumapili, 19 Aprili 2015

Mwalimu ajinyonga, mtendaji agongwa na kufariki papo hapo


Watu wawili wamekufa mkoani Mara katika matukio mawili tofauti. 
 
Akizungumzia matukio hayo Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Audax Mjaliwa alisema katika Mtaa wa Nyamatare Manispaa ya Musoma, mwalimu Tengeru Mongu (43) wa Shule ya Msingi Igina wilayani Serengeti alikutwa amejinyonga katika chumba cha binamu yake Mauma Machunde.
 
Akisimulia mkasa huo binamu wa marehemu huyo alisema, alipoamka jana asubuhi, alikwenda kumgongea mgeni wake huyo bila mafanikio hali iliyomchanganya na kutoa taarifa kwa majirani waliofika kumsaidia kuvunja mlango.
 
Machunde alisema, baada ya mlango kuvunjwa alimkuta binamu yake akining’inia juu ya dari akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka na sababu za kujinyonga hazijajulikani kwani hakuacha ujumbe wowote. 
 
Mwalimu ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema, marehemu mwalimu huyo alipata uhamisho kutoka Serengeti kwenda Wilaya ya Butiama, uhamisho ambao aliuomba kwa madai kuwa umri alionao anafaa kufanyia kazi maeneo ya nyumbani kwao.
 
Katika tukio jingine basi lililosadikiwa kuwa ni la Kampuni ya Peace Maker katika Barabara ya Bunda - Kiabakari kwenye Kitongoji cha Kibisa, Kijiji cha Nyamisisi, Butiama limemgonga mtembea kwa miguu jana usiku saa mbili usiku na kumsababishia kifo cha papo hapo.
 
Akizungumzia ajali hiyo mtoto wa marehemu, Alfred Kitambara, Veronika Kitambara alisema, baba yake ni Mtendaji wa Kata ya Kyanyari na alipopata ajali hiyo alikuwa akitoka katika mkutano wa kijiji akiwa anaendesha pikipiki.
 
Kitambara alisema, wakati baba yake akiwa njiani alipata ajali ya pikipiki ambapo alipiga simu nyumbani na kumweleza mama yake kuwa amepata ajali ya pikpiki amegonga jiwe akaanguka na kudai kuwa hali yake siyo nzuri hivyo alimtaka mama kwenda kumsaidia.
 
“Wakati mama akiwa njiani alikutana na watu wakisema kuwa basi limemgonga mtu lakini halijasimama sidhani kama mtu huyo atakuwa amepona, kufika katika eneo la tukio alikuta aliyegongwa ni baba lakini pikipiki ilikuwa mbali kwa maana hiyo alikuwa ameiacha akawa anatembea ndiyo akagongwa,” alisema Kitambara mtoto wa marehemu.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea kuchunguza magari ya kampuni hiyo ili kubaini ni gari lipi lililogonga kwa madai kuwa hakuna gari iliyofika kituoni kutoa taarifa hizo.
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa