Uamuzi wa chama tawala nchini Burundi wa kumteua Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena hapo tarehe 26 Juni unaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe,
Waandamanaji wakiwa wamekusanyika mjini Bujumbura kupinga tangazo la CNDD-FDD kumteua tena Rais Pierre Nkurunziza kugombea.
Ni ishara inayohatarisha demokrasia barani Afrika. Kulikoni katika nchi
za maziwa makuu? Viongozi wanazidi kungang'ania mamlaka hawataki
kuyaachia na wanazidi kufarakana na watu wao na wanajiweka mbali na kile wanachokitaka wananchi wao.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameibadilisha katiba ya nchi yake ili kumwezesha kutawala daima . Alipoapishwa mnamo mwaka wa 1986 Museveni alisema kuwa tatizo la bara la Afrika ni kwamba viongozi wake wanakaa madarakani kwa muda mrefu na hivyo kuyaweka mazingira ya kuweza kutenda uhalifu bila ya kuwajibishwa ,kujenga ufisadi na mfumo wa uchumi wa kuwapendelea ndugu na marafiki.
Pia nchini Rwanda na katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,Marais Paul Kagame na Joseph Kabila wanatoa ishara kuonyesha kana kwamba bila ya wao mambo hayawezi kusonga mbele katika nchi zao.
Nchini Burundi chama tawala mwishoni mwa wiki kilimteua Rais Pierre Nkurunziza kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa rais na hivyo kuwania muhula wa tatu. Wapinzani walianza kuupinga uamuzi huo siku nyingi kwani ulionekana unakuja.
Katiba ya Burundi hairuhusu muhula wa tatu. Lakini serikali inatoa hoja ya paukwa pakawa kwamba muhula wa kwanza ambao Rais Nkurunziza aliutumikia hauwezi kutiwa katika hesabu, ati kwa sababu wakati huo hakuchaguliwa na umma bali na Bunge.
Maalfu wakimbilia nchi jirani
Maalfu kwa maalfu ya wananchi wa Burundi wameshaikimbia nchi yao na kwenda katika nchi za jirani kutokana na hofu. Na maalfu kwa maalfu walijitokeza barabarani mwishoni mwa wiki kufanya maandamano mengine. Idara za usalama zilitumia ukatili: waandamanji na polisi walipambana na waandamanaji wasiopungua wawili waliuliwa kwa kupigwa risasi na polisi.
Amani nchini Burundi ambayo bado ni teketeke imo hatarini. Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka wa 1993 hadi 2005, watu 300,000 walikufa nchini humo. Hatari ya mvutano uliopo sasa ya kuitumbukiza Burundi katika vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe ni kubwa.
Hatari nyingine inatokana na tawi la vijana waliopo karibu sana na serikali-Imbonerakure. Vijana hao wanawatishia wananchi wazi wazi, na hatari kubwa zaidi ni kwamba wanazo silaha.
Upande wa upinzani uliususia uchaguzi wa mwaka 2005 kwa sababu kwa mtazamo wa wapinzani hao hapakuwapo msingi wa kuwezesha kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Rais na chama chake cha CNDD-FDD wametawala kidikteta nchini Burundi katika miaka iliyopita. Wapinzani wanazibwa midomo na vyombo vya habari vinatishwa.
Mashirika ya haki za binadamu kama vile Human Rights Watch yameripoti juu ya mauaji ya kiholela, mauaji yanayofanywa kwa sababu za kisiasa na pia yamearifu juu ya wapinzani kukamatwa ovyo. Hayo lazima yakomeshwe.
Lakini kwa bahati mbaya miito iliyotolewa na Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kwa jumla haijasaidia kitu. Sasa inabidi nchi jirani ziingilie kati, lakini ni nani anaeweza kurusha jiwe la kwanza, kwani ukimwondoa Rais Jakaya Kikwete, viongozi wengine wote wanataka kuendelea kungang'ania mamlaka.
Licha ya kuwa nchi ndogo na masikini kabisa duniani, Burundi pia imo katika ajenda ya kisiasa ya jumuiya ya kimataifa. Miito peke yake haitasaidia kitu.
Hatua thabiti lazima zichukuliwe,na kwa haraka, ili mgogoro wa nchini Burundi usiendelee kutokota na kuitumbukiza nchi hiyo katika vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe. La sivyo hapatakuwa na matumaini mema juu ya uchaguzi wa bunge mnamo mwezi wa Mei, uchaguzi wa rais mnamo mwezi wa Juni na kwa mustakabal wa Burundi kwa jumla .
Na hasa katika mwaka huu wa adhimu kwa Afrika ,ambapo bara hilo lilianza kuelekea katika njia nzuri, baada kufanyika uchaguzi ulioleta mabadiliko ya uongozi kwa amani, nchini Nigeria, kinachotokea Burundi ,ni jambo linalosababisha wasi wasi mkubwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni