Alhamisi, 9 Aprili 2015

MFUMUKO WA BEI WATAIFA WAONGEZEKA NCHINI


Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Machi 2015 ambao umefikia asilimia 4.3 leo jijini Dar es salaam. Kushoto niKaimu Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja.

 


Waandishi wa Habari wakiwa kazini, Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakati Mkurugenzi wa Sensa naTakwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Machi 2015.
Pichana Veronica Kazimoto – Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)

 
Na. Veronica Kazimoto, Takwimu.

Mfumuko wa Bei  wa Taifa kwa mwezi Machi 2015 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 4.3 ikilinganishwa na asilimia 4.2 za mwezi Februari kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Akitoa taarifa ya mfumuko huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na badiliko la bei ya bidhaa na huduma kati ya mwezi Machi na Februari 2015.

Amesema bei ya vinywaji baridi na bidhaa za vyakula ikiwemo Mchele, Ungawa Muhogo, nyama, Samaki, Maharage, Choroko na Sukari kwa mwezi Machi imeongezeka kidogo ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Februari.

Amesema Mfumuko wa Bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.7 mwezi Machi ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.6 za mwezi Februari huku Fahirisi za bei kwa mwezi Machi zikiongezeka hadi 155.88 kutoka 154.83 za mwezi Februari, 2015 kutokana na ongezeko la bei ya mchele, Samaki, matunda aina ya machungwa, maharage, mboga mboga na sukari.

Aidha, amefafanua kuwa kiwango cha Mfumuko wa bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwezi Machi  2015 kimeongezeka hadi kufikia asilimia 5.9 ikilinganishwa na asilimia 4.9 ya mwezi Februari 2015.
Akitoa ufafanuzi kuhusu uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kwa mwezi Machi 2015 amesema kuwa umepungua na kufikia shilingi 64 na senti 15 ikilinganishwa na shilingi 64.59 za mwezi Februari 2015.

Kwa upande wa mfumuko wa Bei wa mwezi Machi kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema una mwelekeo unaofanana Uganda ikiwa na Mfumuko wa Bei wa asilimia 1.90 kutika  asilimia 1.4 za mwezi Februari huku Mfumuko wa Bei nchini Kenya kwa mwezi Machi 2015 ukiongezeka hadi kufikia asilimia 6.31 kutoka asilimia 5.61 za Februari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa