Diwani wa kata ya Mlangali Mh.Faraja Mlelwa
Hii ndiyo sola aliyoitoa kwa wananchi wa kijiji cha Lufumbu
Wananchi wakishangilia baada ya kukabidhiwa sola na Diwani Mlelwa
Wananchi wa
kijiji cha Lufumbu kata ya Mlangali wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe
wamempongeza diwani wa kata hiyo kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA Mh.Faraja Mlelwa kwa kutoa
msaada wa Sola katika Zahanati ya kijiji hicho ambapo awali walishindwa kupata
huduma nyakati za usiku kutokana na kutokuwa na nishati ya umeme.
Akitoa
shukrani hizo wakati diwani huyo akikabidhi sola hiyo Bi.Teresia Mtweve ambaye
ni mjumbe wa serikali ya kijiji kupitia chama cha mapinduzi ccm alisema kuwa
wagonjwa wamekuwa wakipata taabu nyakati za usiku hasa akina mama wajawazito
kukosa huduma ya matibabu kutokana na kukosa umeme hivyo sola hiyo ni ukombozi
mkubwa kwao.
Bi.Taresia
alisema kuwa katika maendeleo hakuna suala la itikadi ya vyama vya siasa hivyo
kata ya Mlangali imekuwa ikinufaika na mengi kupitia Diwani Mlelwa kwani amekuwa ni mfano wa kuigwa katika
utendaji wake hasa kwa kuwakumbuka akina mama na wazee ambao wanahitaji huduma
ya Afya nyakati zote.
Alisema kuwa
kukosekana kwa nishati ya umeme katika Zahanati hiyo kulisababisha wagonjwa
hasa nyakati za usiku kusafiri hadi katika vijiji jirani ili kuweza kupata
huduma za matibabu lakini hali ilikuwa mbaya zaidi pale msimu wa mvua unapofika
na wagonjwa kushindwa kuwaishwa katika Zahanati jirani na mauti kuwafika
wanaposhindwa kusafiri kutokana na mvua kubwa zinazonyesha nyakati za usiku.
“Tunamshukuru
Mh.Mlelwa kwa kutusaidia hii sola maana itakuwa mkombozi kwetu hasa akina mama wajawazito
kwani tumekuwa na shida sana wakati wa kujifungua hasa usiku waganga
wanashindwa kufanya kazi na giza hali inayosababisha vifo kwa baadhi ya
wagonjwa wa kawaida na akina mama kwa sasa hatutahangaika tena kutafuta
bodaboda usiku kwani ikinyesha mvua ndio tatizo zaidi hatuwezi
kusafiri”,alisema Bi.Teresia.
Naye mganga
mkuu wa Zahanati ya Lufumbu Dkt.Wolfram Kiowi alisema kukosekana kwa umeme
katika Zahanati hiyo kulisababisha baadhi ya Dawa kama chanjo ya Mama na Mtoto
kutohifadhiwa hapo kwani majokofu ya kuhifadhi dawa hizo yanahitaji umeme hivyo
kwa sasa dawa hizo zitahifadhiwa hapo na kuwawezesha wahitaji kupata huduma kwa
urahisi zaidi.
Dkt.Kiowi
alisema Mh.Faraja ameweza kuisaidia Zahanati hiyo kwa mambo mengi likiwemo la
Dawa na Darubini ambavyo alivileta mapema mwaka 2014 na kufanya Zahanati hiyo
kuendelea na upimaji wa vimerea vya magonjwa mbalimbali tofauti na awali
wagonjwa walikuwa wakitibiwa kwa utabiri kwama waganga wa asili.
Alisema kata
ya Mlangali inawasomi wengi kama Mh.Mlelwa hivyo wanapaswa kuwasaidia wananchi
wa kata hiyo kama anavyofanya mwenzao kwani ameweza kuzisaidia Zahanati za
vijiji vyote katika kata ya Mlangali kwa kutoa msaada wa Dawa na Darubini hivyo
amekuwa mfano wa kuigwa na jamii inayomzunguka.
Aidha Diwani
Mlelwa alisema katika uongozi wake ameweza kukamilisha ahadi zake zote
alizowaahidi wananchi katika kampeni zake hivyo aliwataka wananchi kuvitumia
vifaa hivyo kwa umakini ili viweze kuwanufaisha na watoto wa kizazi kijacho
bila kubagua itikadi za vyama vya siasa.
Diwani huyo
ambaye ni Diwani kijana katika Halmashauri ya wilaya ya Ludewa aliingia katika
siasa mwaka 2012 mwishoni baada ya aliyekuwa diwani wa kata ya Mlangali kupitia
chama cha mapinduzi kufa kwa kujinyonga na kamba hivyo ameweza kufanya kazi kwa
miaka miwili na kukubalika kwa kiasi kikubwa na wananchi wa kata yake ambapo
kata hiyo imeshagawanywa na kuwa kata mbili kwa sasa.
Mh.Mlelwa
alisema katika Kampeni zake aliliona suala kubwa linaloisumbua kata ya Mlangali
ni sekata ya Afya na elimu hivyo aliwaeleza wananchi kuwa ataanza na hayo licha
ya kuwa ameweza kuungana na wananchi katika kuibua miradi mbalimbali ikiwemo ya
maji lakini aliyoanza nayo ameweza kuyakamilisha kwa muda muafaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni