Kituo cha radio cha Best FM kinachorusha matangazo yake katika masafa ya 90.5 wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe kiliungana na kauli ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Jakaya Mrisho Kikwete katika suala la ujenzi wa maabara katika shule za Sekondari nchini kwa kutoa fedha taslimu shilingi laki moja kama mchango wa ujenzi huo katika kata ya Ludewa Mjini.
Akikabidhi fedha hizo jana Meneja wa kituo hicho Bi.Deograsia Nyoni alisema kama kituo cha radio kimeguswa na kauli ya Rais hivyo kimeona ni vyema kikashiriki katika michango hiyo inayoendelea kutoka kwa wananchi ambao kila kona ya Tanzania wamekuwa wakishangia kwa lengo la kufanikisha mpango huo ambao unamanufaa kwa kizazi kilichopo na kijacho.
Bi.Nyoni alisema Taifa limekuwa likikosa wataalamu wa Sayansi hivyo kwa mpango huo ni imani yake kubwa sasa watapatikana wataalamu wengi wa sayansi ambao wataweza kuisaidia nchi katika kukuza uchumi kama mataifa mengine ambayo yanawatalaamu wengi wa masuala ya sayansi.
Alisema wananchi wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali katika vipindi vya radio katika mikoa ya Njombe,Mbeya na Ruvuma ambako masafa ya radio best fm yanafika wakiwa na lengo la kuunga mkono mpango huu wa ujenzi wa maabara kila shule ya Sekondari kwani wameona umuhimu wa jambo hili la kimaendeleo hivyo ni vyema kituo hicho kikaungana na wananchi hao katika jambo hilo.
“Sisi kama radio best Fm tumeliona hilo tukalitafakari na kuona Rais wetu ameona mbali na atakumbukwa kwa mengi mazuri katika utawala wake likiwemo na hili ambalo litakuwa faida kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo hivyi nasi tunatoa fedha hii laki moja japo ni ndogo lakini itasaidia pale panapowezekana”,alisema Bi.Nyoni.
Bi.Nyoni aliwataka wadau wengine kama mashirika binafsi na wafanya biashara wilayani hapa kuchangia zoezi ambalo ni mkombozi katika elimu ya Tanzania kwani halijakaa kisiasa bali liko kimaendeleo ya wananchi wote ambao wanahitaji mapinduzi ya kielimu nchini.
Akipokea fedha hizo Ofisa mtendaji wa kata ya Ludewa Bw.Onesmo Haule alisema radio best fm imeonesha uzalendo wa hali ya juu hivyo ni dhahili radio hiyo iliwekwa Ludewa kwa manufaa ya wananchi ili kuwaletea maendeleo na kuwajuza habari za kimaendeleo.
Bw.Haule alisema mpaka sasa wananchi wamekuwa wakitoa michango yao bila ya matatizo kutokana na taarifa sahihi wanazozipata kupitia kituo hicho cha radio hivyo aliwataka wadau wengine kujitokeza kuungana na kituo hicho cha radio ili kukamilisha zoezi hilo katika muda uliopangwa.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni