Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto amesema baada ya kukamilisha shughuli ya ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo Sh306 bilioni zilichotwa, kamati yake sasa inaelekeza nguvu katika kashfa nyingine nne.
Zitto
alisema kamati yake itatumia mwezi huu na Januari kupitia ripoti nne
ambazo zina masilahi kwa Taifa, ikiwamo ya utoaji wa vibali vya kuagiza
na kuingiza sukari nchini.
Alisema ufisadi katika utoaji wa vibali hivyo ni mkubwa kuliko sakata la escrow... “Hili
linagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, wamiliki wa viwanda na
uzalishaji. Tayari tumewaita Bodi ya Sukari tujadiliane kwa kina kuhusu
suala hili,” alisema.
Mbali
na suala la sukari, alizitaja ripoti nyingine kuwa ni ya uchunguzi wa
ubinafsishaji wa Benki ya NBC, ripoti maalumu ya Bandari na mikataba ya
gesi.
“Baada
ya kazi ya PAC, tunapumzika, kwani kama unavyojua kazi ilikuwa ngumu,
wiki mbili nilikuwa silali. Kwa kuwa tuna ratiba ya wiki mbili. Kwa
Desemba na Januari tutaanza kuzifanyia kazi,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Wiki
iliyopita, Bunge lilijadili ripoti ya PAC kuhusu ufisadi katika
Akaunti ya Tegeta Escrow na kuhitimishwa kwa kuweka maazimio manane
yakiwamo ya kuitaka Serikali iwawajibishe baadhi ya mawaziri na
watendaji wengine wakuu huku likitaka pia uchunguzi uendelee kwa wote
waliotuhumiwa kupokea fedha hizo kwa njia moja au nyingine.
Kauli
ya Zitto inakuja wiki moja baada ya wamiliki wa viwanda vya sukari vya
Kagera, Mtibwa na Kilombero kutishia kuvifunga kutokana na kuviendesha
kwa hasara.
Wamiliki
hao walisema watafunga viwanda hivyo kutokana na Serikali kushindwa
kuzuia uagizwaji wa sukari nchini kinyume cha taratibu.
Mkurugenzi
wa Viwanda vya Kagera na Mtibwa, Seif Seif alisema uagizaji wa sukari
kutoka nje unafanyika kwa ushirikiano wa wafanyabiashara wakubwa na
vigogo serikalini kinyume cha makubaliano na hivyo kurudisha nyuma
maendeleo ya viwanda.
“Tulikubaliana
kwamba Serikali iwe inaagiza tani 100,000 kutoka nje lakini sukari
inayoingizwa sokoni ni zaidi ya tani hizo. Sukari tunayozalisha katika
viwanda vyetu ipo na haina pa kwenda,” alisema Seif na kuongeza:
“Leo
ukipita katika maduka utakutana na sukari ya kila aina, wafanyabiashara
wanaoagiza wanawatumia vigogo serikalini kuingiza sukari wapendavyo,
tena bila kulipa kodi,” alisema Seif.
Kutokana
na hali hiyo, Seif alisema wamelazimika kupunguza wafanyakazi 2,000 na
kubakiwa na 5,000 katika Kiwanda cha Kagera, Kilombero imepunguza
3,000 na wamebaki 6,000 huku Mtibwa ikiondoa wafanyakazi 3,000.
“Hali
ni mbaya, si kama Watanzania wanavyofikiri. Tukifunga kabisa Watanzania
wengi watakosa ajira kama ambavyo mnaona wengine wamekosa, hatuwezi
kuendelea kufanya biashara ya hasara ambayo Serikali inaihalalisha,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari Kilombero, Balozi Ami Mpungwe alisema: “Hali ni mbaya, tunaona kuliko kuendelea na hali hii ni bora tusimame kuzalisha sukari.
“Serikali
kama kweli ina dhamira ya kuvifufua na kuviendeleza viwanda vyetu vya
ndani ni lazima kuvilinda na kupiga marufuku uagizwaji holela wa sukari
kutoka nje.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni