Jumanne, 9 Desemba 2014

SERA MADHUBUTI YA GESI KUIPAISHA TANZANIA KIUCHUMI

Mipawa to Ghana

Meneja wa kituo cha Kahama FM Redio, Marco Mipawa (kushoto) akielekea kukwea pipa kuelekea nchini Ghana kwenye ziara ya mafunzo ya wiki mbili.
Na Marco Mipawa, Accra- Ghana
Tanzania inaweza kuwa nchi ya kwanza katika maendeleo ya uchumi iwapo itaweka sera madhubuti za uzalishaji wa Gesi na kuwa na viongozi wenye dhamira dhabiti ya kuiendeleza nchi na kuboresha maisha ya watu.
Haya yamebainishwa na Meneja wa Redio Kahama FM Marco Mipawa leo wakati akiendelea na ziara ya mafunzo nchini Ghana ya kujionea jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi na jamii katika suala zima la maendeleo.
Mipawa ameyasema hayo baada ya kuona kuwa nchi ya Ghana inalo tatizo kubwa la upatikanaji wa nishati ya umeme hata kuliko Tanzania inavyoathirika na tatizo hilo lakini maisha ya watu ni mazuri na uchumi uko juu.
Amesema, katika jiji la Accra umeme hukatika takriban robo tatu ya siku na matumizi ya jenerata ni makubwa lakini thamani ya pesa yao iko kubwa ikilinganishwa na ya Tanzania ambapo kukatikakatika kwa umeme ni mara chache.
Mipawa amesema, dola moja ya marekani inathamanishwa na Sedisi tatu za Ghana ikiwa ni sawa na Shilingi 1770 za Tanzania hali inayoonyesha uchumi wa Tanzania uko chini ukilinganishwa na wa Ghana.
Baadhi ya wananchi wa Accra wamemwambia Mipawa kuwa, kinachoisaidia nchi ya Ghana ni Uzalishaji mali katika kilimo, madini na ufugaji; huku sera na sheria za nchi zikisimamiwa kwa umakini mkubwa kwa maslahi ya nchi.
Wamesema suala la kudhibiti rushwa na kusimamia utii wa sheria vikiambatana na uwazi na ukweli wa serikali na viongozi wa Ghana, ndiyo silaha mahususi zilizoifanya Ghana kuwa na uchumi imara na maisha mazuri ya watu.
Ziara ya mafunzo ya wiki mbili ya kujionea utendaji wa vyombo vya habari nchini Ghana, imehusisha watu tisa kutoka Tanzania wakiwemo waandishi wa habari na viongozi wa vyombo vya habari mbalimbali kwa udhamini wa Tanzania Media Fund (TMF)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa