Azimio hilo la Chadema la kupinga uchaguzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, limetolewa wakati zikiwa zimebaki siku nne tu, uchaguzi huo ufanyike nchini kote.
Katibu wa Chama hicho mkoani hapa, Basil Lema, alisema tayari wamemwagiza Mwanasheria wao kuandaa hoja za kisheria kisha kufungua kesi ya kupinga uchaguzi huo leo kutafuta haki ya wananchi na wagombea wa nafasi mbalimbali walioenguliwa, hivyo kuwakosesha kutimiza haki yao ya kikatiba.
“Jumla ya wagombea 52 wa nafasi mbalimbali wanaotokana na Chadema mkoa wa Kilimanjaro, wameenguliwa kwa makusudi kutokana na kasoro zilizopo kwenye fomu ya kuomba uongozi, lakini pia wamo wapiga kura 517 walioenguliwa na wasimamizi wa uchaguzi kwa madai ya kuwa si wakazi halali na wengine wakitajwa kuwa si raia. Tunaamini wapo wanaoonewa,” alisema Lema.
Katika Kata ya Mawenzi mjini Moshi, wananchi 159 kati ya 162 waliojiandikisha kupiga kura, wameenguliwa baada yakudaiwa kwamba siyo wakazi halali wa eneo hilo. Aidha, kwenye kundi hilo la wanaodaiwa kuwa si wakazi, imo familia ya watu wanne ya Diwani wa Chadema, Hawa Mushi.
Kwa mujibu wa Lema, hali ni mbaya zaidi katika Jimbo la Same Magharibi, kwa kuwa kwenye Kata tatu zenye jumla ya wagombea wake 21 walioomba uongozi wameenguliwa wote na hivyo kutoa mwanya kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa.
“Kwenye jimbo hilo hilo, wananchi 180 wa Kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu wameenguliwa baada ya kujiandikisha kwa madai kwamba wao si wakazi wa eneo hilo. Hizi ni rafu ambazo wenzetu CCM wanatuchezea Ukawa ili kuuhadaa umma kwamba Muungano wetu hauna tija kisiasa,” alisisitiza Katibu huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni